Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amesema kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa wingi wa mapato yaliyokusanywa kwenye mikoa yote kuanzia kipindi cha Julai hadi Machi mwaka huu wa fedha kuwa mkoa huo umekusanya sh. bilioni 118.4.

Ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya tatu (Julai-Machi,2019) kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Amesema kuwa mikoa ya Katavi, Rukwa, Kigoma, Manyara na Lindi imeburuza mkia kwenye ukusanyaji mapato ikilinganishwa na jumla ya makisio kwenye halmashauri za mikoa hiyo.

Aidha ameongeza kuwa mkoa wa Dodoma umeshika nafasi ya pili kwa kukusanya wingi wa mapato yaliyofikia sh. bilioni 57.3, ukifuatiwa na Mwanza (sh. bilioni 22.9), Arusha (sh. bilioni 22.8) na Mbeya ukikusanya sh. bilioni 19.8.

“Mikoa mitano ya mwisho kwa kigezo cha wingi wa mapato yaliyokusanywa ni Manyara (sh. bilioni 6.5), Lindi (sh. bilioni 6.1), Rukwa (sh. bilioni 5.8), Kigoma (sh. bilioni 4.5) na Mkoa wa Katavi (sh. bilioni 3.8),” amesema Jafo.

Waziri Jafo amesema kuwa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam nayo imeongoza kwa kigezo cha asilimia ambapo imekusanya asilimia 87 ya makisio, wakati Jiji la Dodoma likiongoza kwa kigezo cha wingi wa mapato kwa kukusanya sh. bilioni 50.

Aidha amesema halmashauri ya jiji la Tanga imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 57 ya makisio yake, lakini pia imekuwa ya mwisho kwa kigezo cha wingi wa mapato kwa kukusanya sh. bilioni 8.7,”

Amezitaja Halmashauri tano za mwisho kwa kigezo cha wingi wa mapato ni Halmashauri ya Wilaya ya Madaba iliyokusanya sh. milioni 293.7 na Halmashauri ya Wilaya ya Newala (sh. milioni 268.3).

Zingine ni halmashauri ya Wilaya ya Kakonko (sh. milioni 238.6), Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe (sh. milioni 177.3) na Halmashauri ya Wilaya ya Momba imekusanya sh. milioni 170.4.

Amesema kuwa  Halmashauri ya Mji wa Kondoa imeongoza kwenye kundi la Halmashauri za Miji kwa kigezo cha asilimia ambapo imekusanya asilimia 92 ya makisio yake, huku kwenye kundi hilo Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 12 ya makisio.

Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa kigezo cha wingi wa mapato kwa kukusanya sh. bilioni 5.9 na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ikiburuza mkia kwa kukusanya sh. milioni 293.9.

Jafo amesisitiza kuwa uchambuzi huo umefanyika kwa kulinganisha makisio ya mwaka wa fedha 2018/19 kwa kushindanisha halmashauri hizo, makundi ya halmashauri na kimkoa.

Hata hivyo amesema kuwa wakurugenzi ambao halmashauri zao zimeshika nafasi ya mwisho ni vyema wakajitathimini kabla serikali haijaanza kuchukua hatua.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Aprili 27, 2019
Aliyemshtaki R Kelly kwa makosa ya kingono ashinda kesi