Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, imewahukumu kifungo cha miaka mitano jela, Thadei Parokwa (43) na mke wake Lowema Thadei (34), kwa kosa la kuwakeketa watoto wao watatu.

Mwendesha mashitaka wa Polisi wa mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Mkaguzi wa Polisi, Hamilton Moses amesoma shitaka lililowakabili washitakiwa hao kuwa ni ukatili dhidi ya watoto.

Amesema kuwa kesi hiyo iliripotiwa kituo cha Polisi Orkesmet Machi 19, mwaka jana baada ya kukamatwa watuhumiwa hao ambao walidaiwa kuwakeketa watoto hao kwa bibi yao aliyekuwa Kitongoji cha Kangala Kijiji cha Lobosireti Wilayani humo.

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Lugano Kasebele, baada ya kujiridhisha kwa pande hizo mbili, aliwatia hatiani wazazi hao kwenda jela miaka mitano ama faini ya laki sita na fidia ya laki tisa.

Aidha, alisema kuwa vitendo vya ukeketaji vimekuwa vikifanyika kwa kificho wilayani humo, pamoja na uwepo kwa sheria bado vinaendelea kujitokeza hivyo wanatakiwa kutumikia adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hizo.

Kwa upande wake Hamilton, alimwomba Hakimu wa mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa wahusika kwani vitendo hivi vimekithiri wilayani humo huku madhara yakiendelea kujitokeza.

“Mheshimiwa hakimu vitendo hivi vimekithiri hapa wilayani Kwetu ninaomba utoe adhabu kali kwa wahusika ili iwe fundisho kwa wengine kwani vina madhara makubwa kwa jamii” amesema Hamilton.

Zitto Kabwe bado ahitajika Polisi
Raia waandamana mbele ya Ofisi ya Rais Tshisekedi