Klabu ya Simba inazidi kufaidika na usajili wa winga hatari waliomsajili kutoa UD Songo ya Msumbiji, Luis Miquissone, ambaye kwa kipindi hiki amekuwa balozi wa klabu hiyo akiitangaza katika jiji la Maputo.

Luis ni miongoni mwa wachezaji wa Simba waliopewa ruhusa ya kurejea kwao baada ya serikali kusimamisha michuano ya Ligi Kuu Bara kwa siku 30 kufuatia kuzuka kwa ugonjwa hatari wa Corona katika nchi mbalimbali duniani.

Taarifa kutoka kwa watanzania wanaoishi nchini Msumbiji, zinasema, Luis amekuwa akipenda kuvaa jezi za klabu hiyo na kuonekana kuwatamanisha rafiki zake hususan wachezaji wenzake aliowaacha UD Songo.

Mtanzania Yassin Maokola anayeishi karibu na ilipo klabu ya UD Songo, alisema amekutana na mchezaji huyo na kumsalimia kwa lugha ya Kiswahili na yeye akionyesha kujua maneno mengi.

“Kinachofurahisha ni kwamba wenzake wanamuona amepata mafanikio kutokana na klabu ya Simba kuwa na sifa kubwa nchini hapo,” alisema.

Alisema, “Kama ujuavyo, hii klabu ya UD Songo ni ndogo sana, imeanzishwa mwaka 1982 pia ina uwanja mdogo kama ule wa Simba unaoingiza watu 2000 tu, hivyo Luis kuonekana akicheza kwenye Uwanja wa Taifa imemletea heshima kubwa.” Licha ya mchezaji huyo kuwa balozi mzuri wa Simba nchini Msumbiji, pia anaonekana anaweza kuisaidia timu yake endapo itahitaji kusajili mchezaji kutoka timu yoyote nchini Msumbiji.

Simba imekuwa ikiheshimika sana nchini Msumbiji kiasi ambacho Mwenyekiti wa klabu hiyo, Saide Tuhair alikiri kwamba haitakuwa rahisi kumzuia mchezaji anayetakiwa na Simba kutokana na jinsi anavyofahamu hali nzuri ya kiuchumi iliyonayo, kutokana na ufadhili ya mfanyabiashara maarufu na kijana Afrika, Mohamed Dewji ‘MO’

Miquissone tayari ameshafunga Simba mabao matatu, ytangu aliposajliwa klabuni hapo wakati wa dirisha dogo la usajili mwishoni mwa mwaka jana, akifunga dhidi ya KMC mabao mawili na bao moja kwenye mchezo dhidi ya Biashara United.

Corona Kenya: Wafungwa waachiwa kupunguza msongamano
Mtoto wa Malkia Elizabeth aambukizwa Corona