Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewasimamisha kazi Maofisa watatu wa halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani humo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 600 ambazo hazikuwakilishwa kama mapato ya halmashauri kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2018.

Ubadhirifu huo umebainika katika kikao maalum cha kamati ya fedha na mipango ya halmashauri hiyo ambacho kilikuwa kinajadili taarifa ya kamati iliyoundwa na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Meja Jenerali Mstaafu Salim Mustafa Kijuu ambaye amestaafu.

Aidha, maofisa waliosimamishwa kazi ni Alexander Bashaula ambaye ni muweka hazina wa halmashauri hiyo, Salanga Mahendeka Mhasibu na Emmanuel Maleo ambaye ni ofisa ushirika, wote wakituhumiwa kupoteza fedha na kukiuka viapo vya uaminifu.

“Zaidi ya shilingi millioni 690 hazikuwasilishwa kama mapato ya halmashauri kuanzia Agosti mwaka 2016 hadi Mei 2018, huku shilingi millioni 427 hazikuwasilishwa benki na wakusanya mapato,” amesema Bregedia Jenerali Gaguti.

Hata hivyo, Bregedia Jenerali Gaguti ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuanza kuchunguza ubadhirifu huo wa mali ya umma pamoja na kufuatilia hatua za kuwachukulia wahusika kisheria.

Magari matano yateketea kwa moto
Jeshi la Polisi lasweka ndani Kijiji kizima Mbeya