Michuano ya Ligi ya Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ambae pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara imefikia tamati jana toka ilipoanza mwanzoni mwa mwezi Agost 2019, kwa timu ya Kata ya Nyakahanga kuchukua ubingwa huo katika msimu wa pili wa ligi, baada ya kuifunga timu ya Kata ya Kamagambo kwa penalti 3-2 Katika Uwanja mpya wa Bashungwa uliopo mjini Kayanga Wilayani Karagwe Mkoani Kagera.

Kilele cha mashindano hayo  kilitanguliwa na mchezo wa awali wa  mshindi wa tatu kwa kuzikutanisha Timu za kata ya Nyakabanga na Kayanga, ambapo Nyakabanga wameibuka kidedea kwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Kata ya Kayanga baada ya Timu hizo kutoshana Nguvu kwa Dakika 90 za mchezo.

Mgeni rasmi katika mchezo wa Fainali hizo, Constantine Kanyasu, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii amesema amefurahishwa na Fainali hizo hasa umati wa mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo.

Amesema hiyo ni ishara ya upendo mkubwa wa wananchi hao dhidi ya Mbunge wao pamoja na michezo kwa ujumla, licha ya mambo mengine Kanyasu amesisiitiza juu ya Vijana na wananchi kuendelea kutangaza Utalii kupitia michezo hususani hifadhi mbili za Burigi – Chato na Ibanda – Rumanyika zilizopo katika Wilaya za Karagwe na Kyerwa.

Kwa upande wake Mwenyeji na muandaaji wa  mashindano hayo  Mbunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Luga Bashungwa, amewashukuru wote waliofanikisha mashindano hayo kubwa akizidi kumshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo amekuwa akimsaidia kwa kumuunga mkono.

Huku akiongeza kuwa kupitia michezo ataendeleza mshikamano na mahusiano kati ya Vijana na Serikali, ikiwa pia michezo ni ajira, afya na Utalii.

 

Bingwa wa michuano hiyo Timu ya Nyakahanga wameibuka na Kitita cha Shilingi

Tsh 2,500, 000/=, jezi seti 1 na Kombe,

Mshindi wa pili amejipatia Tsh 1,650,000/= na jezi seti 1.

Mshindi wa tatu amejipatia Tsh 450,000/= na jezi seti 1.

Mshindi wa nne amejipatia Tsh 300,000/ na jezi seti 1, huku Zawadi hizo zikinogeshwa na Zawadi kutoka Kwa Mgeni rasmi Aliyeongeza Laki mbili Kwa Mshindi wa kwanza na pili, wakati Mke wa Waziri Bashungwa Mama Alaska akiongeza Milioni Moja katika Zawadi za washindi .Zawadi nyingine ni Timu yenye nidhamu imejipatia jezi seti 1, Zawadi nyingine zilikuwa za:

Golikipa bora, Mfungaji bora na Mchezaji bora kila mmoja amejinyakulia Tsh 50,000/=

 

Kupitia mashindano hayo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brig. Jen. Marco Gaguti ametangaza mechi kati ya Bukoba combine na Karagwe Combine mchezo utakaochezwa wiki tatu zijazo na Mshindi atazawadiwa Milioni Mbili, na atakaeshindwa atapata kifuta jasho shilingi Milioni Moja.

 

Awali ligi hiyo ilishirikisha timu zote za kata  23 zilizopo Wilaya ya Karagwe huku kila timu ikipewa seti moja ya jezi na mpira mmoja kwa ajili ya michuano hiyo.

 

Zimbabwe: Tembo 55 wafa kwa kukosa maji ya kunywa
Patrick Aussems aundiwa mkakati kuhama Simba