Michezo miwili ya raundi ya sita za Ligi Kuu ya soka Tanzania bara kati ya Simba na Majimaji, na African Lyon na Kagera Sugar sasa zitachezwa kwenye Uwanja wa Taifa badala ya Uwanja wa Uhuru.

Mabadiliko hayo yametokana na Shirikisho la soka nchini TFF kusitisha kwa muda kuutumia Uwanja wa Uhuru katika kipindi hiki ambacho limeanza kufanyia marekebisho sehemu ya uwanja huo ambayo ni ya nyasi bandia (artificial turf).

Hivyo basi, mchezo wa Simba na Majimaji utafanyika Jumamosi, Septemba 24 wakati ule wa African Lyon na Kagera Sugar utachezwa Jumatatu, Septemba 26.

Jumapili, Septemba 25 Uwanja Taifa utatumiwa kwa mchezo wa timu za Wabunge za Simba na Yanga ili kuchangia waathirika wa janga la tetemeko lililotokea mkoani Kagera.

Michezo mingine ya ligi Kuu ya soka Tanzania bara itakayochezwa Jumamosi, Septemba 24 ni kati ya JKT Ruvu na Mbeya City (Mabatini), Ndanda na Azam (Nangwanda Sijaona), Tanzania Prisons na Mwadui (Sokoine), Mtibwa Sugar na Mbao (Manungu).

Jumapili kutakuwa na mchezo kati ya Stand United na Yanga (Kambarage), na Ruvu Shooting na Toto Africans kwenye Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.

Kutokana na marekebisho yanayofanyika Uwanja wa Uhuru, mechi ya kundi ya A ya Ligi Daraja la Kwanza kati ya Ashanti United na Pamba iliyokuwa ichezwe Ijumaa, Septemba 23 kwenye uwanja huo sasa itafanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

John Bocco Mchezaji Bora Mwezi Agosti
Sakata la viwanja Kibaha, Waziri Mkuu atoa onyo