Rwanda imetoa malalamiko yake juu ya hatua za maafisa wa usalama wa Uganda kuwakamata raia 40 wa Rwanda jijini Kampala, katika oparesheni iliyotekelezwa na maafisa wa ujasusi kutoka jeshini.

Vyombo vya usalama vya Uganda vimesema kuwa raia hao wamekamatwa kwa tuhuma za kuifanyia ujasusi serikali ya Rwanda.

Wakati huohuo uongozi wa jeshi la Polisi nchini humo umekataa kuzungumzia suala hilo, licha ya msemaji wa polisi jijini Kampala kuthibitisha kwenye vyombo vya habari kwamba jeshi hilo linawashikilia raia hao.

Katika mahojiano ya simu na Sauti ya Amerika, msemaji wa polisi jijini Kampala, Patrick Onyango, amesema kuwa kwasasa hana uwezo wa kuzungumzia suala hilo na kuwaelekeza kwa msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Richard Karemera.

Kwa upande wake balozi wa Rwanda nchini Uganda, Frank Mugambage tayari amewasilisha malalamiko kwa serikali ya Uganda na kusema kuwa ukamataji huo ni dhihaka na unahatarisha mahusiano baina ya nchi hizo.

Naye mchambuzi wa siasa na usalama anayefuatilia masuala ya Rwanda na Uganda, Charles Rwomushana, amesema kuwa ni vigumu kwa taarifa kutolewa kwa sasa.

Aidha, raia hao 40 wa Rwanda, walikamatwa katika Kanisa la Pentecostal Association Churches of Rwanda ADEPR, ghorofa ya kwanza, kwenye chumba kilichokuwa sehemu ya burudani.

Hayo yanajiri wakati uhusiano kati ya Rwanda na Uganda ni mbaya, kiasi kwamba mpaka kati ya nchi hizo mbili umefungwa, ambapo serikali ya Uganda inadai kuwa Rwanda ina njama za kupindua utawala wa Yoweri Museveni kabla ya uchaguzi mkuu wa 2021, huku Rwanda nayo ikidai Uganda inampango wa kupindua utawala wa Paul Kagame.

 

Nyoka awashukia wabunge kwenye kikao, watimua mbio
Rais Magufuli achangia Sh 400 milioni kujenga kituo cha afya kijijini