Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza amesema kuwa mzozo wa wazi kati ya taifa lake na taifa jirani na Rwanda katika kinachoonekana kuwa kudorora zaidi kwa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili unahitaji suluhisho.

Rwanda na Burundi zimekuwa na uhasama kwa muda mrefu sasa, ambapo Burundi imekuwa ikiituhumu Rwanda kwa kuhusika katika jaribio la kupindua serikali mwaka 2015 ambalo lilifeli.

Burundi imedai kuwa Rwanda iliwafadhili waliohusika na kwamba imetoa hifadhi kwa wahusika wa tuhuma za kutaka kupindua utawala huo huku Rwanda ikikanusha tuhuma hizo.

Aidha, Rais Nkurunzinza amemwandikia barua mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Yoweri Museveni ambaye ni rais wa Uganda akisema Rwanda sasa si mshirika tena ndani ya jumuiya bali ni kama adui.

“Rwanda ndiyo nchi pekee katika ukanda huu ambayo ndiyo moja wa wahusika wakuu katika kuvuruga uthabiti wa taifa langu na kwa hivyo siichukulii kama taifa mshirika, lakini kama adui wa nchi yangu,” barua hiyo, ambayo inaonyesha ilitiwa saini na Nkurunziza tarehe 4 Desemba, imesema.

Kiongozi huyo anataka kufanyike mkutano maalumu wa EAC wa kujadili mzozo huo kati ya Rwanda na Burundi ambao umeuwa ukifukuta kila siku.

Hata hivyo, Viongozi wa mataifa ya Jumuiya hiyo ambayo kwa sasa inajumuisha Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na Sudani Kusini wamepangiwa kukutana tena 27 Desemba.

Korosho zote zitabanguliwa nchini - Waziri Hasunga
Mbaroni kwa kumhonga RC majani ya chai ya kichina