Mwanaume mmoja raia wa Japan mwenye umri wa miaka 35 anajitambulisha kuwa baba wa watoto 38 na kuweka rekodi ya kuwa baba wa watoto wengi zaidi duniani mwenye umri kama wake!

Yuichi Ishii, amewapata watoto hao kupitia kampuni yake ya ‘Family Romance’ inayofanya kazi ya kukodisha ndugu wa aina mbalimbali ambao wanawahudumia wateja kama baba, mama, mjomba, shangazi, kaka na wengine.

Hivyo, uhusiano huwa sio halisi bali unatengenezwa kama huduma.

Ishii ameiambia BBC kuwa hadi sasa amefanikiwa kuwa baba bora wa watoto alionao kupitia kampuni hiyo ambao amekuwa akitumia muda wa saa nne kila siku kukaa nao ili kuwapa huduma ya ‘ubaba’ inayowafaa.

Amesema watoto hao wanatoka katika familia 25 ambazo yeye hakuwa na uhusiano halisi na wahusika, bali amechukua jukumu la kutoa ukaribu wa baba. Kutokana na hali hiyo, ana wake zaidi ya 100, lakini batili.

Kampuni yake ya Family Romance imekuwa maarufu na hivi sasa ina wafanyakazi zaidi ya 2,200 na inasifika kwa kutoa huduma ya undugu.

Wazo la Yuichi Ishii kuanzisha kampuni hiyo kwa mujibu wake, lilizaliwa miaka 14 iliyopita ambapo rafiki yake wa karibu alitakiwa kumpeleka mtoto wake shuleni kwa ajili ya usaili ambao ulihusisha pia wazazi wote wawili.

Anasema yeye ilimbidi ajidai kuwa ndiye baba mzazi wa mtoto huyo na walifanyiwa usaili, lakini hawakufaulu kutokana na yeye na mtoto kushindwa kuigiza vizuri kama mtu na baba yake.

“Njia hii haikufanikiwa kama tulivyotegemea kwa sababu mtoto na mimi hatukuweza kuigiza kuwa familia. Lakini nikafikiria kuwa kuna jambo zuri kuhusu suala la uhitaji wa familia,” BBC wanamkariri.

Akizungumzia huduma wanazotoa, alisema kuwa wanajifanya marafiki wa kweli, wana watoto wanaowakodisha, wajukuu na hata wazazi ili kufidia nafasi za watu wenye uhitaji wakati huo.

“Tunakwenda nao kufanya manunuzi, kufanya mazungumzo yanayoleta furaha pamoja na hata kujadili masuala ya kifamilia pamoja,” alisema.

Aidha, alisema kuwa kutokana na uzoefu wa kampuni hiyo, nafasi ya baba ndiyo inayohitajika zaidi ya nafasi nyingine kutoka kwa wateja wake.

Hata hivyo, anasema kuwa huwa anapata wakati mgumu pale mkataba wake wa kuwa baba wa familia fulani unapoisha na kulazimika kuwaaga watoto ambao mara nyingi huwa wanalia wakisikia neno ‘kwaheri’.

Baba huyo wa karne ya 21 ameongeza kuwa moja kati ya changamoto za kazi yake ni kuhakikisha anafuatilia kwa karibu maelekezo na majina ya kila familia na anakutana nao na kuhudhuria vikao muhimu.

“Kuna wakati najikuta nasahau majina yao hasa ya utani. Hivyo, inabidi niende pembeni kidogo nijifiche nipitie tena kitabu changu chenye maelekezo,” anaeleza.

Kuna fursa nyingi duniani zinazozalishwa kutokana na changamoto zilizopo, najua wengi kwa utamaduni wetu tulikuwa tunashangaa kusikia kuna waombolezaji wanakodishwa na sasa tunashuhudia yanafanyika mbele ya macho yetu.

Na hili la kukodi ndugu huenda likatufikia siku moja. Dunia haiishi maajabu, sasa kila kitu ni biashara!

Video: Mnada mali za Mbowe waacha deni, Kaka yake Lissu ajitenga na uchaguzi mdogo
Deni la Bil. 1 lazidi kumtafuna Mbowe, mali zake zapigwa mnada