Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe amezungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, akidai tume ya uchaguzi inapaswa kufanyiwa marekebisho.

Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliamua kumfukuza uanachama na sasa anasubiri uamuzi wa mwisho wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, aliandika kwenye mtandao wa Twitter madai yake huku akidokeza kuwa ndicho alichozungumza pia alipohojiwa na Kamati ya Udhibiti na Nidhamu/Maadili.

“Nilisema hili katika kamati ya maadili na ngoja niseme tena; hali ya kisiasa inayoendelea inathibitisha umuhimu wa kuwa na Tume ya Uchaguzi ambayo ni huru, yenye uwakilishi na inayoendeshwa kwa uwazi katika ngazi ya kitaifa na ile ya chini,” aliandika.

Membe alithibitisha kuwa ujumbe huo ni wake alipofanya mahojiano na gazeti la Mwananchi jana, Machi 19, 2020.

Alifafanua kuwa tume huru ya uchaguzi anayoihitaji ni yenye uwakilishi wa wajumbe wa vyama vingine vya siasa. Alieleza kuwa kwa mazingira ya sasa Msimamizi wa Uchaguzi kwenye jimbo ni Mkurugenzi wa Halmashauri/Manispaa/Jiji ambao amedai wanaweza kupoteza kibarua chao endapo wapinzani wakishinda.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alikutana na mabalozi wa nchi mbalimbali na kuwahakikishia kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na haki. Aidha, alieleza kuwa wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali wataalikwa kushuhudia demokrasia ya kweli nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alikuwa nchini Marekani na kuwasilisha ujumbe wa Rais Magufuli kwa Rais Donald Trump.

Profesa Kabudi alihakikisha kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na haki.

CORONA: Mwanamuziki mkongwe Aurlus Mabele afariki dunia, kifo chake kina mengi
CORONA: Idadi ya vifo Italia yazidi China, 427 wafariki kwa siku