Mchungaji maarufu jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, Alph Lukau leo amezua gumzo baada ya kuonekana kwenye ibada ya Jumapili asubuhi akimfufua mtu aliyedaiwa kufariki tangu Ijumaa, tukio lililooneshwa mubashara kupitia runinga.

Kupitia kipindi hicho cha ibada cha kanisa la Allelujah Ministry linaloongozwa na Mchungaji Lukau, inaonekana wakati wa kipindi cha maombi yaliyotanguliwa na somo la ‘miujiza’, mchungaji huyo anaitwa ghafla nje ya kanisa.

Baada ya kutoka nje anakutana na kundi la waombolezaji wakiwa na jeneza ambalo ndani yake walieleza kuwa kulikuwa na mwili wa mpendwa wao waliyemtaja kwa jina la Elliot, aliyefariki tangu Ijumaa, na kwamba wamemtoa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Mchungaji Lukau anawahoji watu hao kwa kutumia kikuza sauti, akiwa anajiamini na kutoa maelezo zaidi ya msisitizo wa tukio hilo lilivyokuwa, kabla ya kuanza maombi maalum, akiushika ‘mwili wa Elliot’.

“Huyu ni mke wa marehemu… njoo mama. Hawa ni nani, ndugu zake!? Wanasema alifariki tangu Ijumaa na kwamba wamemtoa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema Mchungaji Lukau, na kuanza kufanya maombezi.

Ghafla! Mwili huo unainuka kuashiria kuwa marehemu amefufuka na watu wote wakaonesha mshangao mkuu.

Familia ya Elliot inaonesha kuzidiwa na furaha. Kweli ndugu yao karejeshewa uhai wake!!

Tukio hilo limezua gumzo kubwa, maswali mengi pamoja na kejeli zimechukua asilimia kubwa kuliko majibu na idadi ya wachache ambao wameonesha kusadiki.

Wengi waliouliza maswali ya kutosadiki wamedai kuwa mdomo wa marehemu hufunikwa hasa endapo alikuwa amehifadhiwa katika jumba la huduma za mazishi maarufu kaa ‘Kings and Queens’. Mtu mmoja ambaye anadai aliwahi kufanya kazi katika jumba hilo ameonesha kushangazwa na namna ambavyo ‘marehemu Elliot’ alionekana ndani ya jeneza.

 

Aidha, Kings and Queens nao wametoa tamko la kukanusha kuuhifadhi mwili wa Elliot, ingawa wamedai kuwa walifuatwa na ndugu zake na kujadili kuhusu huduma za kuhifadhi mwili wa marehemu na mazishi.

Wameeleza kuwa baada ya majadiliano, ndugu hao waliwaeleza kuwa wamepata sehemu nyingine ya kuhifadhia mwili pamoja na huduma za mazishi, hivyo walikodi gari la Kings and Queens kwa ajili ya kusafirisha mwili huo.

“Ndugu wale walitufuata tena na kueleza kuwa wamepata sehemu nyingine ambayo wamekubaliana kwa huduma za mazishi na wangependa kutumia huduma yetu ya usafiri ambayo tuliwapa,” imeeleza taarifa ya Kampuni ya Kings and Queens.

“Hatukuwapa jeneza wala hatukuhifadhi mwili wa marehemu na hakuna sehemu tuliyoandikishana kuhusu hilo,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Kings and Queens.

Video: Mahakama yagoma kukamatwa Lissu, Mgomo wa nyama watikisa Mwanza
Video: Tyga azua gumzo kwenye sherehe ya Floyd  Mayweather