Mbunge mwanamke nchini Kenya, Zuleika Hassan ameondolewa ndani ya ukumbi wa Bunge la nchi hiyo baada ya kuingia na mtoto wake wa kike mwenye umri wa miezi mitano.

Kitendo cha mbunge huyo kuondolewa bungeni kilizua sintofahamu ya muda. Baadhi ya wabunge hasa wanawake walipiga kelele wakionesha kupinga amri hiyo, lakini mwisho wakatoka nje wakimsindikiza mwenzao.

Zuleika aliwaambia waandishi wa habari kuwa alilazimika kuingia bungeni humo na mwanaye kwakuwa alipata dharura ya kifamilia na hakuweza kumuacha nyumbani.

“Nimekuwa nikijaribu kila njia ili nisije na mtoto, lakini leo nimepata dharura; ningefanyaje? Kama Bunge lingekuwa na eneo maalum la kuwaweka watoto wakati tuko kazini, ningeweza kumuweka mwanangu huko,” alisema Zuleika.

Spika wa Bunge, Christopher Omulele alisema kuwa mbunge huyo anaruhusiwa kurejea Bungeni bila mtoto.

Kwa mujibu wa kanuni za bunge hilo, mtu asiyehusika ikiwa ni pamoja na watoto haruhusiwi kuingia ndani ya Bunge bila kibali maalum.

Mwaka 2017, Bunge la Kenya lilitunga sheria inayoweka utaratibu wa kuwa na sehemu maalum za kunyonyeshea watoto katika ofisi za Serikali.

Hata hivyo, Zuleika sio mwanasiasa wa kwanza kuingia bungeni na mtoto na kuwa gumzo.

Mwaka 2018, Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Arden alikuwa kiongozi wa kwanza wa kitaifa duniani kuingia ndani ya Bunge la Umoja wa Mataifa akiwa na mwanaye wa kike mwenye umri wa miezi mitatu, jijini New York, Marekani.

Serikali kubuni mbinu mpya ya ununuzi wa magari
Pinda aigeukia CRDB, ‘tuelekeze nguvu zetu huku’