Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel (CCM) amesema kuwa mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Joshua Nassari tangu alipochaguliwa na wananchi kuwa mbunge ametokomea kusikojulikana na hajui shida za wananchi hao waliomchagua.

Mollel ametoa madai hayo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumapili Desemba 2, 2018 katika uzinduzi wa mradi wa uboreshaji huduma za maji safi na maji taka katika jimbo la Arumeru Mashariki.

“Walifanya makosa na hawatarudia tena 2020 na mimi niko hapa kwa ajili ya kuwasemea ili kuhakikisha shida zao zinatatuliwa,” amesema Mollel.

Aidha, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema Nassari yupo na wananchi wake na anafanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo katika sekta ya elimu na afya.

“Nasari alikuwa anasoma ila kwa sasa amemaliza na anaendelea na shughuli zake za Kibunge, Amina si msemaji wa wananchi wa Arumeru kazi hiyo ni ya wananchi wa Arumeru na kama alitaka kushitaki angewashitaki kwa Rais, mawaziri waliotajwa kutohudhuria vikao vya Bunge.” Amesema Mrema.

Naye mbunge wa Monduli, Julius Kalanga amesema kuwa hata akipewa nafasi kadhaa za kutoa maombi yake ili aweze kusaidiwa katika utekelezaji mara zote angetaja maji kwa sababu wananchi wake wana hali mbaya.

“Mh, Rais tunaomba na sisi utukumbuke katika ufalme wako kwa sababu tuna shida kubwa ya maji, kama ulivyowakumbuka wenzetu wa Arumeru,” amesema Kalanga.

Video: JPM aigeukia TRA, aitaka ijitathmini, 'Sio kupeleka Polisi kuwakamata wananchi'
Serikali yawashusha presha wakulika wa korosho

Comments

comments