Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe pamoja na Mbunge wa chama hicho, Ester Matiko wamemtumia salamu za pole Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye ambaye alipatwa maradhi ya ghafla alipokuwa katika ziara mkoani Tanga

Katika taarifa ya salamu hizo iliyotolewa na chama chake ambapo imesema, “Mwenyekiti Freeman Mbowe ambaye bado yuko mahabusu Gereza la Segerea na Mbunge Esther Matiko, wamemtumia salaam za pole na kumtakia uponaji wa haraka Sumaye ili arejee katika siha njema”

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa Sumaye anaendelea vizuri na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari wa Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) alikohamishiwa baada ya kupokelewa Hospitali ya Taifa Muhimbili akitokea Hospitali ya Mkoa wa Tanga.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Vincent Mashinji, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA, Patrick Ole Sosopi pamoja na viongozi wengine wa Chama ngazi na maeneo mbalimbali ya nchi, wamefika hospitalini hapo kumjulia hali.

Hata hivyo, Sumaye aliugua ghafla alipokuwa ziarani mkoani Tanga ambako alikuwa anaendelea na ratiba ya shughuli mbalimbali za Chama mkoani humo, ambapo alilazwa katika hospitali ya Bombo kabla ya kuhamishiwa Muhimbili jijini Dar es salaam kwaajili ya uchunguzi zaidi.

 

Dkt. Gwajima azitaka timu za Afya mikoani kujitathmini kiutendaji
'Ni wewe' ya Ommy Dimpoz yampigisha magoti Steve Nyerere