Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, ameonesha kutoridhika na uamuzi unaofanywa na jeshi la polisi katika kutekeleza majukumu yake akidai kuwa hufanya upendeleo viongozi wa ngazi za juu wa CCM huku akimtolea mfano rais wa awamu ya pili, Benjamini Mkapa.

Akiongea na waandishi wa habari jana, Mbatia alieleza kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Kipolisi, Suleiman Kova ameshindwa kumchukulia hatua za kisheria Mzee Mkapa kwa kosa lile lile lililowahi kufanywa na askofu Josephat Gwajima aliyechukuliwa hatua kali.

“Gwajima alitoa kauli zilizosemekana kuwa ni za kuudhi dhidi ya Kadinali Pengo, lakini Kadinali alisema amemsamehe. Pengo alimsamehe hadharani laini vyombo vya dola vilimfungulia kesi mahakamani,” alisemaa Mbatia.

“Juzi tumesikia matusi mabaya kuliko ya Gwajima yakitolewa na viongozi wa CCM akiwemo Mkapa, kwa nini yeye hajakamatwa. Kwanini Kova hajamkamata Mkpaa na kumfungulia mashtaka dhidi ya uchochezi,”alisema.

Mbatia alilitaka jeshi la Polisi kuhakikisha linatenda haki kwa kila mmoja na kwamba sheria isipofuatwa vizuri bila ubaguzi inaweza kulipasua taifa.

Aliwataka wanachama wa Ukawa kuwa watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi na kuwa na uvumilivu pia kwa kuwa utulivu na amani ya Taifa ni kitu bora zaidi ya vyama vya siasa.

Katika hatua nyingine, Mbatia alisisitiza kuwa ratiba ya Ukawa kufanya uzinduzi katika uwanja wa Jangwani iko pale ingawa Serikali imelikataa ombi lao la kuutumia uwanja huo kwa madai kuwa tayari umechukuliwa na mtu mwingine.

Lowassa Aja Na Mbinu Mpya Ya Kampeni Kwa Wanawake
Magufuli Aahidi Walimu Maisha Bora Kama ‘Mapadri’