Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameziagiza Taasisi zote za Serikali nchini kuhakikisha zinapeleka taarifa zao kuhifadhiwa katika kituo cha Taifa cha Kuhifadhi kumbukumbu cha Kijitonyama (IDC) kwani kituo hicho ni salama na kina ubora wa hali ya juu katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Aidha, amezitahadharisha baadhi ya Taasisi zenye mpango wa kujenga na  kuanzisha vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu kuacha mara moja mpango huo,  kwani kufanya hivyo ni kuingilia kazi ya kituo hicho na kupoteza fedha za Serikali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa,mapema hii leo mara baada ya kutembelea kituoni hapo na kupokea taarifa ya uendeshaji wa kituo hicho kutoka kwa Mkuu wa Kituo.

“Sioni sababu kwa Taasisi nyingine kutaka kujenga vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu, Serikali imeshawekeza fedha nyingi kwaajili ya ujenzi wa kituo hiki, hivyo taasisi zote nchini zinalazimika kutumia kituo hiki”,  amesema Profesa Mbarawa

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo hicho Abdul Mombokaleo, amesema kuwa hadi sasa wameshafanikiwa kuunganisha wateja 13 kujiunga na kituo hicho na wengine zaidi ya 40 wapo katika mchakato wa kujiunga.

#HapoKale
Video: Nchi haijakumbwa na baa la njaa - Majaliwa