Zile purukushani za mashabiki wa Manny Pacquiao na timu yake kumuamsha tena bondia ambaye hajawahi kupoteza, Floyd Mayweather zimefanikiwa na ameamua kuwapa wanachotaka.

Mayweather ambaye alitangaza kustaafu baada ya kumaliza pambano lake na Conor McGregory mwaka jana, ametangaza kurudi tena ulingoni Disemba mwaka huu kupigana na Pacquiao.

Wababe bao ambao awali walipigana Mei 2015, ambapo Mayweather alimshinda Pacquiao kwa alama za majaji kwa mbali, walikutana Jumamosi uso kwa macho katika tamasha la muziki jijini Tokyo na kuwekana sawa.

Katika vipande vya video vinavyosambaa mtandaoni, Mayweather na Pacquiao wanaonekana kuzungumza na baadaye kutambiana hadharani.

“Disemba narudi, Disemba narudi,” Mayweather anasema kwa mbwembwe mbele ya Pacquiao. “Ni rahisi, ni rahisi…” anaongeza.

Pacquiao ambaye ni Seneta nchini kwake ameweka kipande hicho cha video kwenye Twitter na kuandika (50-1 #NoExcuses), akimaanisha kuwa atampiga Mayweather na kumuwekea alama ya kushindwa mara moja kwenye rekodi yake ya 50-0, bila kuwa na sababu.

Mayweather pia ameweka kwenye Instagram kipande cha video kwenye Instagram yake na kuandika, “ninarudi kupigana na Manny Pacquiao mwaka huu, malipo mengine ya tarakimu 9 kwa siku yako njiani.”

Katika pambano lao la Mei 2015, Mayweather alishinda akipokea malipo ya $220 Milioni. Pacquiao pia alipokea zaidi ya $160 milioni katika usiku huo na kuwafanya kuwa wachezaji walioingiza fedha nyingi katika mwaka huo. Inaaminika kuwa katika pambano lao la marudio wataweza kuingiza kiasi kikubwa zaidi.

Pacquiao anashikilia mkanda wa ubingwa wa dunia baada ya kumpiga Lucas Matthysse mwaka huu. Mayweather ameahidi kuuchukua.

 

 

 

 

 

CCM wakomaa na ushindi Monduli, Ukonga
Canelo ampiga Golovkin, matokeo yazua utata tena