Mtakwimu mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa amesema Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na matumizi bora ya takwimu zinazozalishwa na ofisi ya Taifa ya takwimu (NBS).

Akizungumza jana, Jijini DodomaJijini Dkt. Chuwa amesema ofisi hiyo imefanikiwa kuzalisha takwimu zenye ubora wa viwango vinavyokubalika kimataifa hali inayochochea mafanikio chanya ya miradi inayotekelezwa.

“Matumizi sahihi ya takwimu zinazopikwa na NBS ni chanzo cha Serikali ya awamu hii kufanikiwa katika utekelezaji wa miradi na tunatarajia kujenga ofisi katika mikoa yote hapa nchini ili kuboresha zaidi mfumo wa ukusanyaji takwimu,” amessistiza Dkt. Chuwa.

Amesema takwimu bora ni msingi wa maendeleo yaliyofikiwa hapa nchini katika sekta zote zinazolenga kuleta ustawi wa nchi na kwamba kwa kuongeza ofisi hizo kutaiwezesha Serikali kupanga mipango yake kwa ufanisi.

Kuhusu utekelezaji wa mpango wa taifa wa kuboresha na kuimarisha takwimu (TSMP) kwa awamu ya pili Dkt. Chuwa amesema unalenga kufanya maboresho mbalimbali katika ukusanyaji na uchakataji wa takwimu na kujenga miundombinu bora hadi ngazi ya mikoa.

“Katika malengo ya millenia lengo namba 17 linasisitiza ushirikiano kati ya Serikali na wadau kwa lengo la kuchochea maendeleo ya wananchi na ndio maana ili kufanikisha makusudio haya tumekuwa na ushirikiano nao wakiwepo Benki ya Dunia,” amefafanua Dkt. Chuwa.

Awali mchumi mwandamizi kutoka Benki ya Dunia Nadia Belhaj Hassine Belghith amesema Tanzania ni nchi ya mfano wa kuigwa kutokana na maendeleo yaliyofikiwa kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na miundombinu kutokana na matumizi ya takwimu zenye viwango na ubora unaotakiwa.

Amesema takwimu ni msingi na kichocheo cha maendeleo katika taifa lolote na kuongeza kuwa Tanzania ambayo katika Afrika ni ya pili kwa kuzalisha Takwimu Bora inafanya vizuri maana hata wakulima ili wapate masoko ya bidhaa zao na pia huzitumia.

“Ili wakulima wajue ni wapi yalipo masoko ya mazao yao ni lazima wawezeshwe na takwimu na hali hiyo huchochea maendeleo yao binafsi na nchi kwa haraka zaidi kwani kutakuwepo na mwamko baada ya kufahamu ni wapi wanatakiwa kupeleka bidhaa zao ili kufanya mauzo,” amesisitiza Bi. Belghith.

Benki ya Dunia na ofisi ya Takwimu NBS wamekutana Jijini Dodoma katika mkutano wa mashauriano wa kuimarisha ushirikiano baina yao ambapo wamejadili ufanikishwaji na utekelezaji wa mpango kabambe wa pili wa Taifa wa kuboresha na kuimarisha Takwimu (TSMP II).

Mpango huo unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia 2019/ 2020 hadi 2024/ 2025 baada ya kumalizika kwa hatua ya mwanzo ya majadiliano na uboreshaji iliyofanyika Juni, 2018.

Video: Vita mpya Lugola vs Kigogo, Wiki tatu za mnyukano
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Novemba 3, 2019

Comments

comments