BAADA ya Rais John Magufuli kuruhusu michezo yote kuendelea kuanzia Juni Mosi, Promota wa ngumi za kulipwa hapa nchini Ally Mwanzoa amesema ataandaa mapambano na la kwanza litafanyika Julai 7 mwaka huu.

Promota huyo ameuambia mtandao wa Timesmajira kuwa, mapambano hayo yatakuwa ya ndani na sasa wanaangalia uwezekano wa kuanza kufanyika kati ya jijini Dar es Salaam au Tanga.

Mbali na mapambano hayo ya Julai 7 lakini pia Agosti 8 huenda kukuawa na pambano lingine litakalohusisha pia mabondia kutokana ndani ya nje ya nchi.

Amesema, sababu kubwa za mapambano hayo kuanza kufanyika Julai ni kuwapa mabondia muda wa zaidi ya mwezi mmoja wa maandalizi ya nguvu ili kurudi katika viwango vyao.

“Kwa mabondia ni lazima wapate zaidi ya mwezi mmoja wa mazoezi ili yaweze kuwaingia baada ya kukaa muda mrefu bila mazoezi ya nguvu hivyo naamini kuwa baada ya muda huo watapanda ulingoni Julai 7 na Agosti 8 ili kupambana,” amesema Mwanzoa.

Hata hivyo amesema kuwa, baada ya mapambano hayo, mwezi Desemba watafunga mwaka na mapambano ya usiku ya mabingwa ambayo yalitakiwa kufanyika miezi iliyopita lakini wakalazimika kuahirisha kutokana na uwepo wa virusi vya ugonjwa wa Corona (COVID-19) jambo lililopelekea Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kusimamisha shughuli zote za michezo kwa zaidi ya miezi miwili.

Awali pambano hilo la kimataifa litakalowakutanisha mabingwa wa ndondi wa Tanzania na wapinzani wao kutoka nje ya lilipangwa kufanyika Machi 28 lakini lililazimika kupelekwa mbele hadi siku ya Pasaka, Aprili 12 kutokana na bondia Hassan Mwakinyo kukabiliwa na pambano la kimataifa nchini Ujerumani.

Katika pambano hilo lililopangwa kufanyika Machi 21, mwaka huu la kuwania ubingwa wa WBO ‘International Super Welter Weight’ dhidi Jack Calcuy ambalo nalo lilishindwa kufanyika baada ya ugonjwa huo kuzikumba nchi nyingi Duniani.

“Awali tulipeleka mbele mapambano haya ili kumpa Mwakinyo nafasi ya kujiandaa na pambano lake la Machi 21 ambalo nalo liliahirishwa kutokana na ugonjwa wa Corona, lakini sasa tunajipanga kivingine na mapambano ya Julai, Agosti na lile la kufunga mwaka litakalofanyika Desemba,” amesema Mwazoa.

Katika mapambano hayo ya mabingwa, Mwakinyo atapamba ulingoni kutetea ubingwa wa UBO na WBF (Mabara) katika pambano litakalokuwa na raundi 12.

Mbali na bondia huyo, bingwa wa mkanda wa WBO uzito wa Super Middle Asian Pacific, Abdallah Pazi, ‘Dulla Mbabe’ atapamba ulingoni kugombea ubingwa wa UBO katika pambano la raundi 10.

Kwa upande wake, Twaha Kiduku atashuka ulingoni kupambana katika pambano la raundi 10 kuwania ubingwa wa ‘International UBO na WBF Lakini pia mabondia wa Tanzania Salim Mtango na Francis Niyeyusho nao watapanda ulingoni kuzichapa.

Mosimane azima kelele za kuikacha Sundowns
Tetesi za usajili barani Ulaya