Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri Hector Cuper, amepingana na baadhi ya mashabiki wa nchi hiyo wanaotoa sababu za kufanya vizuri kwa timu yao kwenye fainali za kombe la dunia zinazoendelea nchini Urusi, kupitia kivuli cha mshambuliaji Mohamed Salah.

Misri imeshindwa kujihakikishia nafasi ya kuingia kwenye hatua ya 16 bora ya fainali hizo, baada ya kufungwa mabao matatu kwa moja na wenyeji Urusi usiku wa kuamkia leo, na kuwa timu ya kwanza kuondoshwa kwenye michuano hiyo japo wamesaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Saudi Arabia.

Baadhi ya mashabiki wa Misri wamedai kuwa, kutokuwepo kwa Mohamed Salah katika mchezo wa awali dhidi ya Uruguay, ilikua sababu kubwa ya kikosi chao kushindwa kufanya vizuri, hasa baada ya kuonyesha soka safi na kukubali kufungwa dakika za lala salama.

Mashabiki hao wanaamini endapo Salah angekuwepo kwenye mchezo huo, huenda Misri wangefanikiwa kupata matokeo mazuri, kutokana na pengo la mshambuliaji huyo wa klabu ya Liverpool kuonekana mara kwa mara.

Akizungumza mara baada ya mchezo wa jana dhidi ya Urusi, kocha Hector Cuper alisema haamini kama kweli kukosekana kwa Salah katika mchezo wa kwanza dhidi ya Uruguay imekua sababu ya kikosi chake kushindwa kufanya vyema, na kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora.

Kocha huyo kutoka nchini Argentina alisema anaamini kilichotokea ni makosa waliyoyafanya katika michezo yote miwili, na sababu inayotolewa na baadhi ya mashabiki hao ni sawa na kujificha kweye mgongo wa mshambuliaji huyo, ambaye alikua akikabiliwa na majeraha ya bega la mkono wa kushoto kwa majuma matatu yaliyopita.

“Siamini kama kutokuwepo kwa Salah katika mchezo wetu wa kwanza ndio sababu ya kushindwa kufikia lengo, wachezaji wangu wamefanya makosa katika michezo yote miwili na tumeadhibiwa kutokana na udhaifu wetu,” alisema Cuper.

“Kimtazamo unaweza kusema tulicheza vizuri katika michezo yote miwili (dhidi ya Uruguay na Urusi) lakini makosa madogo madogo yametugharimu kwa kiasi kikubwa.

“Mfano mchezo wetu wa leo (Jana) wachezaji wangu walionyesha udhaifu katika kipindi cha pili na wenzetu walitumia nafasi hiyo kutuadhibu jambo ambalo huwezi kusema kukosekana kwa mchezaji fulani ndio sababu ya kilichotufika.”

Kikosi cha Misri ambacho bado hakijavuna alama yoyote kwenye msimamo wa kundi A, kitamaliza michezo ya kundi hilo mwanzoni mwa juma lijalo kwa kucheza dhidi ya Saudi Arabia.

TCRA yadai haijakaa kimya kuhusu matapeli wa mitandaoni
Bunge laiweka kitimoto serikali, laitaka kutoa maelezo kwa kina