Ikiwa bado kuna sintofahamu kuhusu maisha ya kampuni ya Fastjet Tanzania baada ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kusitisha uendeshaji wake, Kampuni hiyo imeahidi kuingiza ndege nyingine wiki hii.

Akizungumza jana kupitia Clouds TV, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni hiyo, Laurent Masha amesema kuwa Jumamosi hii kampuni hiyo itaingiza ndege moja na baadaye zitangia ndege nyingine mbili kubwa.

“Baada ya kukamilisha kuingia kwa ndege mpya Jumamosi hii, tunatarajia kungiza ndege nyingine mbili aina ya Boeing 737-500 ili kuongeza idadi ya safari zetu. Hivyo, tutaondoa changamoto ya kuahirishwa kwa safari,” alisema Masha.

“Ndege zote zitakazoingia zitasajiliwa hapa Tanzania. Na kadiri ambavyo mahitaji ya ndege yatakavyoongezeka, tunatarajia kununua ndege mbili nyingine aina ya Bombardier,” aliongeza.

Fastjet Tanzania ambayo ilikuwa ikimiliki asilimia 45 ya soko la usafiri wa anga nchini iliporomoka hivi karibuni ikikabiliwa na ukata. Pigo la kiuchumi limelikumba shirika hilo lililofanya kazi kwa mafanikio kwa takribani miaka saba nchini, hali iliyosababisha TCAA kuagiza ndege za Fastjet kutosafirisha abiria.

Masha ameeleza kuwa wanaendelea kufanya mazungumzo na Mamlaka hiyo ili wapate ruhusa ya kuanza kuuza tiketi zao.

Kikwete ampa tano Mwana FA, ‘nilimshauri’
Video: Magufuli afuta ndoto za fidia, Bodi ya mikopo yakusanya bil. 15 kwa mwezi

Comments

comments