Mshambuliaji kutoka nchini Colombia, Jackson Arley Martínez Valencia, anaamini kusajiliwa kwake kwenye kikosi cha Atletico Madrid ni hatua nzuri kwa klabu hiyo ya mjini Madrid, kurejesha heshima ya kutwaa tena ubingwa wa nchini Hispania msimu ujao wa ligi.

Martinez, alieleza matarajio hayo, wakati aliposalimiana na mashabiki 10,000 waliokua wamejitokeza kwenye uwanja wa Vicente Calderón, katika shughuli ya kutambulishwa.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, amesema usajili wake anaamini utaongeza nguvu katika mipango ya klabu hiyo ya kuhakikisha wanarejesha heshima baada ya msimu uliopita kupokonywa ubingwa wa La Liga na FC Barcelona.

Hata hivyo amewataka mashabiki kuwa na uvumilivu pale mambo yatakapokwenda mrama katika msimu mpya wa ligi ya Hispania lakini akasisitiza wazi kwamba lengo ni mafanikio kwanza na mengine yatakayojitokeza katika safari yao yatachukuliwa kama majaribu.

Wakati wa shughuli ya kutambulishwa mbele ya mashabiki, baadhi ya manazi wa Atletico Madrid walishindwa kujizuia kwa furaha na kujikuta wakiruka uzio na kuingia kwenye sehemu ya kuchezea ili wakamilishe azma ya kumshika mshambuliaji huyo kitendo ambacho kilifanikiwa kabla ya maafisa wa usalama hawajawaondoa uwanjani.

Martinez, amejiunga na Atletico Madrid kwa usajili wa paund million 25 akitokea FC Porto ya nchini Ureno.

Mkongo Mangulu Atua Newcastle United
Stevan Jovetic kuitosa Man City