Kocha wa timu ya taifa ya Italia Luigi Di Biagio amefungua milango ya kumrejesha kikosini mshambuliaji Super Mario Balotelli ambaye kwa sasa anacheza soka katika ligi ya nchini Ufaransa.

Di Biagio ameliweka wazi jambo hilo alipozungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalum wa kuelekea katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki, ambapo kikosi cha Italia kitapambana na Argentina siku ya ijumaa.

Kocha huyo amesema anaridhishwa na kiwango cha Balotelli, lakini suala la kumuita litategemea na uwezo wake utakavyoendelea kuimarika siku za usoni.

“Idadi ya mabao yake inavyoendelea kuongezeka, ninaanza kushawishika kumuita katika kikosi cha timu ya taifa, lakini jambo hilo litategemea na juhudi zake kwa siku za usoni,”

“Nimemfutilia katika michezo kadhaa, nimeona namna alivyobadilika kwa kila hatua ambayo siku za nyuma kila mmoja alidiriki kumnyooshea kidole, lakini ninaamini yote hayo yatajidhihirisha siku za usoni, kwa mujibu wa mtihani niliompatia wa kuongeza bidii anapokua uwanjani.” Amesema Di Biagio.

Balotelli amekua na kiwango kizuri akiwa na klabu yake ya Nice ambayo imeonyesha kuwa na ushindani wa kweli katika ligi ya nchini Ufaransa, tangu ilipomsajili mwanzoni mwa msimu wa 2016/17.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, tayari ameshafunga mabao 22 katika michezo 31 aliyoitumikia klabu ya Nice, kwenye michuano yote aliyocheza msimu huu.

Kwa mara ya mwisho Balotelli aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Italia wakati wa fainali za kombe la dunia za 2014 zilizofanyika nchini Brazil.

Kikosi cha Italia kitapambana na Argentina mjini Manchester siku ya Ijumaa, na siku nne baadae kitacheza dhidi ya England katika uwanja wa Wembley.

Michezo hiyo itakua ya kwanza kwa kikosi hicho tangu kiliposhindwa kufuzu fainali za kombe la dunia za 2018, zitakazounguruma nchini Urusi kuanzua Juni 14.

Uwanja wa Samara (Cosmos Arena) bado haujakamilika
Uingereza yaruhusu mtoto kupewa bangi