Serikali ya Marekani imesema inatambua juhudi za Serikali ya Tanzania za kuvutia wawekezaji na kwamba Mazingira mazuri ya uwekezaji yanayofanywa na Serikali yatasaidia kufikia Uchumi wa kati na wa Viwanda.

Hayo yamesemwa na Kaimu Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Dkt. Inmi Patterson ambapo amesema kuwa, kufuatia juhudi hizo Serikali yake inaungana na Tanzania katika kuwezesha wawekezaji wengi wa Kimarekani kuja kuwekeza Nchini.

Ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Geoffrey Mwambe alipomtembelea Ofisini kwake na kuzungumzia masuala mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo namna bora ya kuvutia wawekezaji wa nje.

“Ubalozi wa Marekani, nchi ya Marekani na Wamarekani wote waliopo nchini Tanzania wapo tayari kusaidiana na serikali katika kuhakikisha nchi ya viwanda inafanikiwa,” amesema balozi Patterson

Aidha, ameishauri Serikali ya Tanzania kuwa ili ifanikiwe kwenye uchumi wa viwanda ni vyema ikaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kufanikisha uwekezaji na kwamba amefurahishwa na mazungumzo ambayo ya Serikali ya Tanzania inafanya kati yake na sekta binafsi.

Kwa upande wake Mwambe amesema TIC jukumu lao ni kukutanisha sekta mbalimbali za Serikali na binafsi ambapo mabalozi wa Tanzania waliopo nchi mbalimbali wanahakikisha wanashiriki kikamilifu kuvutia wawekezaji.

 

Ujerumani kudhamini tamasha la Sauti za Busara
Waziri apinga ushauri wa watu kupunguza ulaji wa nyama

Comments

comments