Vyombo vya usalama katika Jimbo la Florida nchini Marekani, vimemkamata Graham Ivan Clark, kijana mwenye umri wa miaka 17, anayetuhumiwa kudukua akaunti za Twitter za watu maarufu na mashuhuri wakiwemo Barack Obama, Elon Musk, Bill Gates na Kanye West.

Clark anatuhumiwa kwa makosa 30 likiwemo la udukuzi na atashtakiwa kama mtu mzima pamoja na watu wengine wawili waliokamatwa naye.

Zoezi hilo la udukuzi anaodaiwa kuufanya, umeathiri zaidi ya akaunti 130 na kuwafanya wateja kuanza kupata mashaka ya usalama kupitia mtandao huo.

Kijana huyo ambaye hajafikisha umri wa utu uzima, anadaiwa kudukua akaunti za makampuni makubwa na kujaribu hata kudukua akaunti ya Bitcoin.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, amepangiwa dhamana ya $725,000.

Mwanasheria wa Serikali amesema kuwa kijana huyo mdogo ana kiasi cha $3 milioni kwenye Bitcoin.

Kiasi hicho cha dhamana alichopangiwa ni mara sita zaidi ya kiwango alichokuwa amepangiwa mwezi uliopita, alipotuhumiwa kufanya wizi wa mtandaoni.

Katika tuhuma hizo ambazo vyombo vya usalama vilidai kuwa vilibaini Julai 15, 2020, anadaiwa kuiba kiasi cha $117,000 kupitia mfumo wa fedha wa ‘cryptocurrency’, ndani ya saa chache.

Magaidi wavamia gereza, wapambana vikali na walinzi
TAKUKURU yaokoa Sh. 170 Milioni zilizopigwa na ‘wajanja’ - Rukwa