Uongozi wa Klabu ya Manchester United umemuwekea kifua Kocha Jose Mourinho dhidi ya tetesi kuwa huenda kibarua chake kikaota nyasi baada ya kupokea kipigo kisichotarajiwa cha 3-2 dhidi ya Brighton, Jumapili.

Matokeo hayo yalisababisha mti wa Mourinho kupigwa mawe kila kona na mashabiki wa klabu hiyo, huku Zinedine Zidane akitajwa kuwa mtu anayefikiriwa kuchukua nafasi ya kukinoa kikosi hicho.

Chanzo kutoka kwenye uongozi wa Man Utd kimetupilia mbali tetesi hizo kikieleza kuwa, “kwanini tufanye majadiliano na Zidane wakati hakuna nafasi ya kazi?”

Mourinho huenda anakingiwa kifua kutokana na ukweli kuwa klabu hiyo haikuyafanyia kazi maombi yake ya kutaka aongezewe bajeti na kuruhusiwa kufanya usajili zaidi wa wachezaji watakaoziba mianya aliyoilenga.

Mourinho alitahadharisha wakati wa usajili kuwa timu yake itakuwa kwenye wakati mgumu kwenye Ligi Kuu kama haitaimarisha ngome yake kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.

Kocha huyo alitaja eneo la ulinzi kama eneo ambalo linahitaji kuimarishwa zaidi, lakini hadi hadi dirisha hilo linafungwa maombi yake hayakufanyiwa kazi.

Baada ya kipigo cha Jumapili kilichozua mjadala, kocha huyo msema mengi alieleza kuwa timu yake ilifanya makosa mengi ya kiufundi na makosa hayo yalikuwa muhimu na fursa kwa wapinzani wao.

Katika mchezo huo, magoli ya Man Utd yalifungwa na Romelu Lukaku (dakika ya 34) na Paul Pogba (dakika ya 90+5’). Genny Murray, Shane Duffy, na Pascal G ndio walioongoza safu ya Brighton kupeleka kilio Man Utd.

NBS kujenga kituo kimoja cha Takwimu za Afya
Jeshi la Polisi nchini Uganda lakamata waandamanaji 103