Meneja wa mabingwa wa soka nchini England (Manchester City) Pep Guardiola, amesema kikosi chake hakipo tayari kutwaa ubingwa wa Ulaya msimu huu.

Guardiola amefichua siri hiyo, baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa mapambano hususan katika safu ya ushambuliaji, ambayo mwishoni mwa juma lililopita, ilifanikiwa kupata mabao mawili dhidi ya Crystal Palace kwenye mchezo wa ligi ya England.

Gabriel Jesus na David Silva waliifungia Man City mabao hayo ya ushindi katika uwanja wa Selhurst Park, na kuendelea kuifanya labu hiyo ya Etihad Stadium kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, kwa tofauti ya alama sita dhidi ya vinara Liverpool.

Kwenye mchezo huo Jesus alifikisha bao lake la 50 tangu alipoanza kuitumikia Man City mwaka 2017 akitokea Palmeiras, lakini alikua na uwezo wa kufunga mabao mengi zaidi siku hiyo ya Jumamosi.

Guardiola amesema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, hakua makini wakati wote, na kama angetulia, angeweza kuweka rekodi kupitia mchezo dhidi ya Crystal Palace.

“(Jesus) bado ni kijana dogo,” Alisema Guardiola kuwaambia waandishi wa habari. “Tulipoteza nafasi nyingi za wazi. Tunapaswa kujirekebisha katika hili, ili kufanikisha lengo la kutwaa ubingwa wa barani Ulaya, kutokana na sababu hiyo imenidhihirishia kuwa, hatupo tayari kufanya hivyo kwa msimu huu… tunapaswa kujiimarisha kwanza.”

Hata hivyo Man City inaongoza kwa kuwa na mabao mengi ya kufunga tangu walipoanza msimu huu, wameshafunga mabao 29, ambayo yanaleta tofauti ya mabao saba dhidi ya vinara wa ligi Liverpool.

Jesus alipewa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza dhidi ya Palace, akichukua nafasi ya mshambuliaji kutoka Argentina Sergio Aguero, ambaye alipata tatizo la ajali ya gari alipokua akielekea mazoezini siku ya Jumatano juma lililopita.

“Ukimfananisha Jesus na Sergio utaona kuna vitu viwili tofauti… lakni Gabriel ni mstahamilivu,” aliongeza Guardiola. “Kila tunapokua katika uwanja wa mazoezi amekua akijitahidi kupambana ili kujiimarisha zaidi.”

Man City wanatarajia kurejea uwanjani kesho Jumanne, kucheza dhidi ya Atalanta ya Italia ambayo itafunga safari hadi Etihad Stadium, kwa ajili ya mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya makundi.

'Boxer' tayari kuwavaa waarabu
Mafuriko yafukua makaburi, Tanzania yavuna Barrick