Chama cha Walimu Tanzania CWT kimetoa shilingi milioni 12 kwa walimu wastaafu 32 kutoka maeneo tofauti tofauti wilayani Njombe ili kuwatia moyo kutokana na kazi waliyokuwa wakiifanya wakati wa utumishi wao.

Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hiyo katika hafla fupi ya kuwaaga walimu hao iliyofanyika katika ukumbi wa chama hicho uliopo mjini Njombe mwalimu Thobias Sanga ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji taifa, amesema kuwa wameamua kutoa fedha badala ya kuwakabidhi bati kama ilivyozoeleka kutokana na makubaliano yao kwa kuwa wengi wao wamekwisha jenga.

Aidha, ametoa wito kwa wastaafu kupumzika na kuto kuanzisha kazi mpya kutokana na umri walionao badala yake kuendeleza miradi waliyokuwa nayo ili kuepuka kujiingiza katika gharama zisizokuwa za lazima.

“Naamini wote mlijiandaa kisaikolojia lakini ni muhimu mkawe wastaafu msije kuanzisha kazi mpya mkapumzike, tumeshuhudia wapo wastaafu wanaokwenda kuanzisha shule au maduka na kwenda kukimbizana, kazi hizo ni za vijana mtaumia,” amesema Sanga

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Njombe Shabani Ambindwile amesema kuwa chama kitaendelea kupambana, kuwatetea na kutatua matatizo sugu ya walimu ikiwemo kupandishwa kwa madaraja.

Nao baadhi ya walimu waliostaafu wamesema kuwa kustaafu ni kwa mujibu wa sheria hivyo wameishukuru serikali huku wakishauri kupunguzwa kwa muda wa ustaafu ili mtumishi aondoke akiwa na nguvu.

Chama hicho kimekabidhi shilingi laki tatu na elfu arobaini na saba kwa kila mwalimu badala ya bati ishirini walizotakiwa kukabidhiwa waalimu hao.

Idara ya wazazi CCM mkoa wa Njombe watoa elimu kwa Vijana
Video: Ruge alinisaidia kabla hata ya kuanza kazi CloudsFm- Fredy

Comments

comments