Milioni mia tatu kati ya bilioni moja na milioni mia nne na themanini na tano zilizokuwa mikononi mwa watu na kusababisha benki ya wananchi Njocoba iliyopo mkoani Njombe kufilisika, zimeanza kurejeshwa kutokana na hatua kali zilizoanza kuchukuliwa na kamati iliyoundwa na Mkuu wa mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka amesema jumla ya kiasi hicho cha fedha Kimeanza kurejeshwa kwa kikosi kazi kilichoundwa Octoba 23 2019 na kutoa siku 14 ili kuweza kuwafikia wadaiwa wote wasio waaminifu waliosababisha kufilisika kwa benki hiyo.

“Kwa muda wa wiki mbili kikosi kazi hiki mpaka jana jioni kimekusanya shilingi milioni mia tatu na wananchi wapatao 71 walikuwa wamemaliza kabisa madeni yao, 49 waliweza kuripoti katika kikozi kazi wakalipa sehemu ya fedha wanazodaiwa na wameingia kwenye mikataba ya kulipa fedha zilizosalia,hadi sasa tuna wananchi wapatao wapatao 216 ambao bado kikosi kazi hakijawafikia”alisema Ole sendeka.

Aidha amebainisha kuwa baada ya kukamilika kwa siku 14 na kufanya tathmini ya zoezi hilo wameweza kupokea maombi ya wananchi na wadaiwa wengi wakiomba kuongezewa muda wa kulipa madeni yao, hivyo wameongeza muda mpaka Novemba 30 mwaka huu ili kutoa nafasi ya wadaiwa waweze kumalizia madeni yao.

Katika hatua nyingine Ole Sendeka amewataka wadaiwa walio mbali na makao makuu ya mkoa kuripoti katika ofisi za wakuu wa wilaya na kuwasilisha fedha zao zitakazowasilishwa mbele ya kikosi kazi na baadaye kuwasilishwa katika akaunti ya mfilisi.

Mpaka sasa deni lililobaki ni bilioni moja na milioni mia moja na themanini na saba huku jumla ya wadaiwa wote wa benki ya maendeleo ya wananchi Njombe Njocoba wakiwa 336 huku 71 wakiwa wamemaliza madeni yao, 49 wameingia kwenye mikataba na kikosi kazi huku 216 wakiwa bado hawajafikiwa na kikosi kazi.

LIVE KIBAHA: Maadhimisho Siku ya Malaria nchi za SADC
Mpango wa Taifa maendeleo sekta ya fedha wapikwa