Mama Mzazi wa marehemu Golden ‘Godzilla’ Mbunda ameomba nyimbo kadhaa za injili alizoimba mwanaye kuwekwa msibani ili kila mtu azisikie.

Kwa mujibu wa mama, Godzilla amewahi kumsikilizisha nyimbo takribani tatu za injili (gospel tracks) zilizokuwa bado zinaendelea kukamilishwa studio.

Kwa mujibu wa Simulizi na Sauti, Mama Zilla alizungumza na Fredrick ‘Skywalker’ Bundala ambaye mbali ya kuwa ni jirani yake, alikuwa rafiki yake pia.

“Mama alikuwa ananiambia ‘God [Godzilla] alikuwa akinipeleka studio nisikilize nyimbo zake’. Na mama anaonekana alikuwa shabiki mkubwa wa nyimbo zake na alimpa matumaini na kumtia moyo,” alisema Skywalker.

“Mama [Godzilla] aliniambia kuwa aliposikiliza nyimbo za Godzilla za gospel alizipenda na akamshauri kuwa ahamie kwenye muziki wa aina hiyo na kwamba atabarikiwa, lakini Godzilla alionesha kutokubaliana moja kwa moja na wazo la mama,” aliongeza.

“Kwahiyo mama alikuwa akinisisitiza kuwa ‘mtafuteni yule mwenye studio anyonye zile nyimbo alete zipigwe hapa, tena ngoja nihamishe kabisa godolo nipeleke nje nisikilize nyimbo za mwanangu,” Baby Sky, mke wa Skywalker alisimulia pia.

Hata hivyo, walieleza kuwa baada ya tafakuri waliona halikuwa wazo zuri kwani nyimbo hizo zingemuongezea uchungu zaidi mama wa msanii huyo.

Godzilla maarufu pia kama King Zilla alifariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitai ya Lugalo alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa ya familia, mkali huyo wa ‘Mama I made It’ atapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele Jumamosi wiki hii.

Msiba wa rapa huyo umesababisha majonzi mazito kwa wadau wa muziki nchini. Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa waliomlilia msanii huyo.

Dar24 tunaendelea kuungana na wadau wa muziki nchini kutoa pole kwa familia ya King Zilla. Mungu ampumzishe kwa amani.

Zitto akumbuka ugomvi wake na Lissu, ‘alisema tumemwaga sana damu zetu’
Mavunde asheherekea Valentine's Day kwa kutoa misaada

Comments

comments