Naibu Waziri wa kazi na ajira na mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga ambaye jana alitangaza kuihama CCM akidai kutotendewa haki na chama hicho katika kura za maoni, ameweka wazi kile alichokiita chuki dhidi yake kwa kuonesha upendo kwa Edward Lowassa.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya kutangaza uamuzi wake wa kujiondoa katika chama hicho na kuomba nafasi ya kujiunga na Chadema, Makongo Mahanga alieleza kuwa kigogo mmoja wa CCM waliwahi kumuita na kumuonya  asiwe karibu na Edward Lowassa ambaye alikihama chama hicho hivi karibuni na kupewa nafasi ya kugombea urais kupitia Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa.

“Niliambiwa na kigogo mmoja wa CCM kwamba wewe uking’ang’na kuwa karibu na Lowassa, hakika hautapanda cheo,” alisema.

Mahanga amesisitiza kuwa yeye na Lowassa ni marafiki wa karibu kiasi cha kushiriki mara kwa mara chakula nyumbani kwake kama rafiki wa familia.

Katika hatua nyingine, Mahanga ameutuhumu uongozi wa CCM wilaya ya Ilala kwa kupanga njama na kumhujumu katika mchakato wa kura za maoni kutokana na ukaribu wake na Lowasssa, hujuma ambazo zimezaa matunda na kumkosesha ushindi.

“Kawaida ukiingia, mwanachama unakatiwa karatasi moja unakwenda pembeni unatick. Lakini unakuta wakati wa kuhesabu kura, fungu la makaratasi yaliyokuwa yamebanwa pamoja kama 10, 15 hadi 20 yametumbukizwa pamoja. Ina maana kwamba hazikupigwa kura mojamoja na wala haikuingizwa karatasi moja ambayo ilikuwa hakupigwa na mtu mmoja,” Mahanga alisimulia.

Aliongeza kuwa timu ya mawakala wake walifanikiwa kuzishika baadhi ya karatasi hizo huku nyingi zaidi zikiwa zimehesabiwa kwa ‘bao la mkono’.

Magoli Ya Mkono Yatawala Kura Za Maoni, Makamba, Ndugai, Nchemba Watajwa
Dk Slaa: Sipedi Siasa ya Unafiki