Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, ametangaza mpango kabambe wa kuviwezesha vikundi vya mazoezi ya kukimbia (jogging club) kwa kuweka utaratibu wa mashindano ya kila mwisho wa mwezi.

Ambapo kikundi kitakachoshinda kitapatiwa kiasi cha shilingi milioni 10 kama mtaji wa kufanya shughuli za kujikwamua kiuchumi.

Hatua hiyo imekuja baada ya Makonda kubaini idadi kubwa ya vijana hao wakimaliza mazoezi asubuhi hawana shughuli ya kufanya hivyo wanakaa vijiweni.

”Vijana wengi wa ‘Jogging Club’ hizo wanafanya mazoezi asubuhi halafu hawana kazi za kufanya wanarudi vijiweni, hiyo si salama maana unaweza ukashangaa wakajikuta wameanza kuwa na ‘speed’ kubwa na matokeo yake wakapita na mikoba ya wakina mama kama hawana kazi za kufanya.

Ameongezea ”Kwa hiyo sisi tunaratibu na kupitia hadhara hii niwaambie wananchi kwamba tunapanga mipango kwa kila mwisho wa mwezi kuwepo na mashindano ‘Jogging Club”, amesema Makonda.

Amesema kitendo cha kukaa kijiweni kinaweza kuwasababishia kushawishika kufanya vitendo vya uhalifu hivyo kwa kuwapatia mtaji itawawezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali utakaowakwamua kiuchumi.

Amesema mashindano hayo yataanza rasmi mwezi ujao, na kwa kuanzia shindano hilo litaanzia wilaya ya Temeke kwa kuwa ndiyo inayoongoza kwa Jogging Club, kwa Dar es salaam, hivyo amezitaka jogging club zote za mkoa kukutana Temeke.

Taesa yatoa ufafanuzi jinsi ya kujisajili ajira 10,000 bomba la mafuta Hoima
Polepole: Zitto Kabwe ajiandae kutafuta kazi ya kufanya