Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli pamoja na wasaidizi wake imeamua kufanya kazi kwa bidii ili kukuza uchumi wake.

Ameyasema hayo wakati alipokutana na Viongozi wa Watanzania wanaoishi nchini Uganda katika hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort jijini Kampala.

Amesema kuwa katika kuleta uchumi wa viwanda, Serikali imedhamiria kuongeza na kuboresha upatikanaji wa Umeme, huduma ya maji, kuboresha mitaala ya elimu, kuboresha huduma za afya pamoja na miundombinu.

Aidha, amewaambia Viongozi hao wa Watanzania wanaoishi Uganda kuwa miradi mingi inayofanyika Tanzania inafanyika kwa kutumia fedha za ndani.

Pia amewataka Watanzania waishio nje ya Tanzania kuja kuwekeza nchini kwani kuna maboresho mengi ya kuvutia wawekezaji yamefanyika.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuna Watanzania zaidi ya milioni 2 wanaishi nchi za nje hivyo amewaomba kuwa mabalozi wazuri wa kuisemea nchi yao.

Kuhitimisha mkutano wa Africa Now Summit 2019, Makamu wa Rais alipata nafasi ya kuchangia katika suala zima la mtazamo wa kijinsia ambapo alisema bado wanawake hawapewi nafasi ya kutosha kwenye mambo mengi ya msingi kuanzia kwenye elimu, uongozi na masuala mengine ya huduma za kijamii.

 

Mambo saba unayopaswa kuyajua baada ya ndege ya Ethiopia kuanguka
Zimebaki siku 14 Kamera Daraja la Mfugale "Fly over" kukamilika