Na Ghati

Leo ikiwa ni siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani. Ni siku ya kuwapa heshima zaidi wanawake ambao wamebarikiwa kuwa chanzo cha maisha ya binadamu. Tukiwa tunaungana na kuwapongeza, tukumbuke jinsi ambavyo wamefanikiwa kubadili dunia na kuwa hii tunayoifurahia leo.

Wanawake wana mchango mkubwa, wao ndio waliogundua programu za mahesabu za kompyuta, ni wanawake ndio waliogundua mionzi na hata upatikanaji wa X-Ray, hawa akina mama ndio waliokuwa wa kwanza kuwagomea wazungu kwa nguvu kubwa zaidi iliyozaa matunda ya kwanza.

Hawa ni baadhi ya wanawake wa chuma walioibadili dunia wakati huo, hata leo wapo:

Ada Lovelace

Ni mwanamke aliyezalia na kukulia Uingereza lakini alibadili maisha ya teknolojia tunayoiishi leo. Ada aliyeishi kati ya mwaka 1815 na 1852, alikuwa mtaalam wa hesabu ambaye anatajwa kuwa aligundua mifumo bora zaidi ya mahesabu yanayoweza kufanywa na kompyuta.

Mtaalam huyu wa mahesabu anatajwa kuwa mtu wa kwanza duniani kugundua mfumo mzima wa kompyuta unaoweza kusaidia kufanya mahesabu, kuchakata data na hata kujibu maswali na kufanya kazi ‘automatically’. Ndiye aliyechapisha mahesabu ya kwanza ya mfumo wa kompyuta. Vitabu vya historia vinamtaja mwanamke huyu kuwa ndiye mtaalam wa kwanza wa program za kompyuta (first computer programmer).

Ada Lovelace

 Marie Curie

Mwanamke huyu pia alileta mapinduzi ya sayansi kwenye eneo la kemikali. Ndiye kiumbe wa kwanza kugundua mionzi (radioactive) na ndiye aliyeipa jina hilo. Kwa wale wakemia mtakuwa mnaifahamu vizuri ‘periodic table’. Basi huyu ndiye mgunduzi wa Radium na Polonium ambazo ni sehemu ya Kemikali, na andiye aliyeipa Radium alama ‘Ra’ na kuwa na atomic namba 88. Aliishi kati  ya mwaka 1867–1934.

Bi. Curie aliweza, ni mwanamke wa kwanza kushinda tuzo ya Nobel, alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa profesa kwenye Chuo Kikuu cha Paris, na kikubwa zaidi, mtu wa kwanza kushinda kwa mara ya pili tuzo ya Nobel.

Hata hivyo, pamoja na kufanya mambo haya makubwa, Bi. Curie ambaye alikuwa mke wa mwanasayansi mwenzake, Pierre alikumbwa na misukosuko mingi. Familia yake ilinyanyaswa na utawala wa Urusi lakini alipambana na kusimama imara.

Akiwa Poland, maswahibu ya utawala wa Warusi yalimfuata. Alipokimbilia Ufaransa alibaguliwa na kunyanyaswa kwa madai kuwa ni mgeni halafu ni mwanamke.

“Kweli wajenzi hawajui mbegu za fito”.

Bi. Curie alikuwa mwanamke wa chuma, imara na asiyeogopa. Wakati wa vita ya Kwanza ya Dunia alitumia usomi na ugunduzi wake vizuri, alisaidia kuhakikisha magari ya wagonjwa (ambulance) yana vifaa vya kutosha ikiwa ni pamoja na mashine za mionzi (X-Ray). Lakini pia, aliingia katika eneo la vita mwenyewe akiwa na ambulance akiwasaidia wahanga.

Kwa bahati mbaya, Bi. Curie alipata ugonjwa kutokana na mionzi aliyokuwa anafanyia kazi. Alipata saratani ambayo ilisababisha kifo chake. Ingawa amefariki, jina na kazi yake vimeendelea kuishi, jamii ya watu wanaopambana na magonjwa ya saratani wameendelea kulitumia jina lake katika kuwatia moyo wagonjwa katika mapambano.

 Rosa Parks, 1913–2005

Huyu ndiye mwanaharakati wa kwanza mwanamke ambaye anatajwa kuwa mtu wa kwanza kupigania haki za kiraia; na Bunge la Marekani lilimbatiza jina la “Mama wa Harakati za Uhuru”.

Bi. Rosa Parks anakumbukwa zaidi kwa kuweka historia ya kugoma kumpisha kiti mzungu kwenye basi la umma. Alitakiwa kumpisha kiti mzungu ambaye alikuwa amekosa nafasi baada ya upande uliotengwa kwa ajili ya ‘wazungu tu’ kujaa. Ingawa hakuwa mtu wa kwanza kugoma, lakini mgomo wake ulikuwa wa aina yake kwani hata baada ya kukamatwa, kusukumwa ndani na baadaye kufikishwa mahakamani akichungulia kifungo kwa kuvunja sheria za kibaguzi za Alabama, alisimama imara.  Kitendo chake kilizaa harakati za kupigania haki sawa, na miaka ya 1960 makundi mengi yalimuunga mkono. Mwisho, wazungu walikubali kutomnyanya mtu kwenye kiti.

Kitendo chake cha kugoma kupisha kiti kwenye basi kiligeuka kuwa ishara ya harakati nyingi dhidi ya ubaguzi wa rangi, na yeye alikuwa mwanaharakati mkubwa wa kimataifa hadi umauti ulipomfika. Miaka mitano baada ya kifo chake, Barack Obama alikuwa mtu wa kwanza mweusi kuwa Rais wa Marekani.

Rosa Parks

Marie Stopes, 1880–1958

Hili ni moja kati ya majina maarufu kwenye afya ya uzazi duniani kote, hata hapa nchini unazisikia sana hospitali za Marie Stopes.

Ni mwanamke aliyeishi kati ya mwaka 1880 na 1958, mzawa wa Edinburgh, Scotland aliyesoma katika Chuo Kikuu jijini London nchini Uingereza. Huyu mama, ndiye mwanzilishi wa harakati za uzazi wa mpango ambazo hadi leo ‘tunahangaika nazo’.  Huyu ndiye chimbuko la ‘Nyota ya Kijani’.

Alifanikiwa kuishawishi sehemu kubwa ya dunia kupitia vitabu vyake viwili vya afya ya uzazi na uzazi wa mpango vinavyoitwa ‘Married Love’ na ‘Wise Parenthood’. Ingawa alipigwa vita na kuzua utata mwingi ambao hadi leo upo kuhusu uzazi wa mpango, Bi. Marie Stopes alifanikiwa kuanzisha kituo cha kwanza cha uzazi wa mpango mwaka 1921, kilichokuwa katika maeneo ya watu masikini, Kaskazini mwa jiji la London.

Leo, mataifa mengi duniani hutumia fedha nyingi kuhamasisha uzazi wa mpango.

Huda Sha’rawi

Huyu ni mmoja kati ya wanawake waafrika walioibadili dunia tunayoiona leo. Akiishi kati ya Juni 23, 1879  hadi Desemba 12, 1947, alikuwa binti wa familia ya kitajiri na ya mwanasiasa mkubwa wa Misri. Lakini alijitoa na kuanza harakati za kupambana dhidi ya unyanyasaji wa Waingereza, na alifanikiwa kuwaunganisha wanawake wengi kupigania haki zao katikati ya msitu wa utawala katili usiodhamini wanawake.

Moja kati ya matukio yanayokumbukwa zaidi ni tukio la baada ya vita ya kwanza ya dunia, mwaka 1919. Sha’arawi alifanikiwa kuratibu mgomo mkubwa kuwahi kutokea nchini humo dhidi ya utawala wa Uingereza, ingawa walilazimishwa kutawanyika, wanawake walisimama wima kwa saa tatu kwenye jua kali. Mwaka 1924 alisababisha mwanamke kupewa nafasi ya kuzungumza kwenye Bunge la Misri akieleza kuhusu haki za wanawake, na hii ilikuwa hatua kubwa ya hali tunayoifurahia leo.

Kwa Tanzania, wapo wanawake wa chuma wengi waliowahi kutokea na waliopo, na mfano mzuri ni Bibi Titi Mohammed, rafiki wa karibu wa Mwalimu Julius Nyerere aliyeshiriki kikamilifu katika ukombozi na mabadiliko chanya ya Tanganyika na Tanzania.

Mwalimu Julius Nyerere akiwa na Bibi Titi Mohammed

Lakini pia wapo wanawake wengi kwenye tasnia ya sanaa na burudani, uchumi na mambo mengine ambao hadi leo wanaendelea kuibadili dunia kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi.

Lakini tusisahau muujiza huu mkubwa ulioibadili dunia kiimani:

Bikira Maria

Aliishi kati ya Karne ya Kwanza kabla ya kuzaliwa Kristo hadi Karne ya Kwanza baada ya kuzaliwa Kristo. Bikira Maria, ndiye anayetajwa kuwa mwanamke maarufu zaidi kuwahi kutokea dunia na bado ataendelea kuwa mwanamke maarufu zaidi.

Vitabu vitakatifu vya Biblia na Quran vinamtaja kuwa ndiye aliyemzaa Yesu Kristo bila kumjua mume. Aliishi Nazareth akiwa mwenyeji wa Galilaya (Galilee) Israel. Ndiye aliyesaidia kubadili dunia tuliyonayo hivi sasa ya kuwa na imani ya Kristo, kwani yeye ndiye aliyemzaa Yesu Kristo. Alifanikiwa kumuona Malaika Mkuu, Gabriel na kuzungumza naye zaidi ya mara moja.

Ni kupitia mama Maria, leo kuna Ukristo.

Nawatakia Heri ya Siku ya Wanawake Duniani. Wanawake wameweza tangu zamani na hadi leo wanaweza.

Kumbuka tu, “Mwanamke mwenye tabia nzuri na uthubutu anaweza kuibadili dunia kwa dakika chache kuwa mahala bora zaidi pa kuishi.”

Video: Wanawake wahimizwa kufanya kazi za Tehama
Waziri Mwakyembe amlilia Kibonde, 'Poleni sana kwa msiba'