Na Josefly

Ulimwengu wa rap/hiphop uliuanza mwezi Aprili mwaka huu kwa majonzi mazito, baada ya kuamka na taarifa mbaya kuwa rapa Nipsey Hussle, kijana mwenye damu ya kiafrika aliyeitikisa Marekani ameuawa kwa kupigwa risasi.

Ni kama rapa huyo alikiona kifo chake siku chache kabla, aliiona nguvu ya maadui wake waliotaka kumtoa roho. Alitumia mtandao wa twitter kuelezea hali iliyokuwa inamkabili.

“Kuwa na maadui wenye nguvu ni baraka,” alitweet.

Hakuna aliyejali sana maandishi hayo hadi taarifa za kifo chake ilipotangazwa.  Polisi walieleza kuwa Eric Holder, kijana mwenye umri wa miaka 29 aliyegombana na Nipsey saa chache Machi 31, 2019, ndiye aliyerudi na kumuua rapa huyo kwa risasi nje ya duka lake la nguo maarufu kama ‘Marathon’ kwenye viunga vya Kusini mwa Los Angeles, katika siku hiyohiyo.

Watu mbalimbali maarufu duniani walionesha kushtushwa na msiba huo, na wengi waliumizwa kwani walijua mgodi wenye madini ya mashairi na ‘flow’ umeanguka.

Nipsey Hussle ni nani?

Mzee Asghedom raia wa Eritrea aliyekimbia vita iliyokuwa inaendelea katika nchi hiyo ya Afrika, alitua nchini Marekani kutafuta maisha. Alikutana na mrembo Lauren London, raia wa Marekani mwenye asili ya kiafrika aliyemliwaza na kumsahaulisha machungu ya vita. Agosti 15, 1985 wakiwa Los Angeles, California, walibarikiwa kupata mtoto wa kiume waliyemuita Ermias.

Ermias alikuwa mtoto mtukutu na mjanja sana. Alikulia katika mitaa ya jiji la Los Angeles. Akiwa kijana mdogo, aliwahi kujiunga na genge hatari la kihalifu la mtaani la ‘Rollin 60’s Neighborhood Crips’. Hili ni genge la kihalifu la mtaani kubwa zaidi Marekani lenye wanafamilia kati ya 6,000 hadi 8,000. Inaelezwa kuwa lilianza miaka ya 1970 likijiengua kutoka kwenye genge la ‘Crips’.

Ermias alikuwa ameanza kuonesha kipaji cha kurap na utukutu wake, rafiki yake mmoja alimbatiza jina la utani akimfananisha na mchekeshaji ‘Julius Nipsey Russle’. Jina hilo lilikuwa, akalibadili kidogo na kuwa ‘Nipsey Hussle’.

“Maisha kwenye genge la uhalifu ilikuwa sawa na kuishi vitani. Tulikuwa tunajihusisha na vifo na mauaji,” Hussle aliiambia Los Angeles Times mwaka 2018.

“Ilikuwa kama kuishi kwenye eneo la vita ambapo watu wanakufa kwenye nyumba hii halafu watu wengine ni kama hawajihusishi na vifo hivyo,” aliongeza.

Mwaka 2005, alibisha hodi rasmi kwenye mkondo mkuu wa muziki wa rap akiachia kandamseto (mixtape) ya kwanza ‘Slauson Boy Volume 1’. Ndani ya kipindi cha miaka mitano, alifyatua mixtape nyingi na jina lake likaanza kuwa gumzo. Mwaka 2010, akawa ameshaeleweka na akashiriki kwenye wimbo mkubwa wa wasanii uliolenga kuisaidia Haiti, ‘We are The World 25 for Haiti’.

Baadhi ya mixtape zake ni pamoja na Bullets Ain’t Got No Name, Vol. 1, 2 na Vol. 3. na mfululizo wa mixtape yake maarufu ya ‘Marathon’ iliyoanza kutoka mwaka 2011. Marathon ndiyo iliyompa nguvu zaidi na hata kulitumia jina hilo kwenye duka lake la nguo.

Jamaa alikuwa halali, alikuwa mtafutaji wa mashairi na aliwavutia wasanii wengi. Katika kipindi hicho alifanikiwa kufanya kazi na wasanii kama Drake, Rick Ross, YG, Snoop Dogg na wengine wakubwa. Kuna wakati tetesi zilienea kuwa angeweza kujiunga na Mayback Music ya Rick Ross, lakini aliishia kushiriki kwenye albam yao ‘Self Made Vol. 2’.

Oktoba 8, 2013, Nipsey Hussle alifanikiwa kufanya tukio zito kupitia mixtape yake rasmi ya nane iliyoitwa ‘Crenshaw’. Ilikuwa moto wa kuotea mbali. Kutoka kwenye mixtape hiyo aliachia ngoma kadhaa kama ‘Face The World’ na ‘Blessings’. Nipsey alitoa nakala 1,000 pekee za mixtape hiyo akiziuza mtandaoni kwa $100 (zaidi ya Sh 230,000 za Tanzania) kwa kila nakala.

Jay Z ni mmoja kati ya walioshikwa na uwezo wa rapa huyu mwenye damu ya kiafrika. Aliamua kununua nakala 100 haraka za mixtape hiyo. Unaambiwa ndani ya saa 24 mzigo wote ulikuwa umekwisha.

Katika kipindi hiki chote alikuwa hajaachia albam yake rasmi, licha ya kuahidi mara kadhaa na kuahirisha. Lakini jina lake lilikuwa linapaa kwenda kileleni kila siku.

Jarida la LA Weekly lilimuweka kwenye jarada lake na kumtaja kuwa ni ‘Next Big L.A MC’. Kwa tafsiri isiyo rasmi ‘ni mchenguaji mkubwa ajaye wa Los Angeles. Jarida la XXL lenyewe lilimuita ‘Most Determined’.

Ucheleweshwaji wa albam yake uliongeza kiu ya mashabiki ambao walikuwa wameshapagawishwa na mixtapes nyingi pamoja na nyimbo chache rasmi za mkali huyo.

Hatiamaye, Februari 16, 2018 aliachia albam yake ya kwanza aliyoibatiza jina ‘Victory Lap’. Albam hiyo iliyosubiriwa kwa miaka 13 ilipata mafanikio makubwa, ikitajwa kushindania tuzo ya Grammy mwaka 2019 kama ‘Albam Bora ya Mwaka’. Hata hivyo, tuzo hiyo ilienda kwa Cardi B na albam yake ‘Invasion of Privacy’.

Nipsey amekuwa akizungumzia mara kadhaa maisha yake ya familia na uhusiano wake na Eritrea.

“Eritrea ndio nyumbani kwetu. Ni sehemu ambayo baba yangu anatoka. Nimewahi kupatembelea na nilipata elimu kubwa ya upande wa pili wa maisha,” Nipsey amewahi kuiambia The Daily Loud.

Baba yake ni rafiki yake mkubwa na mara nyingi amekuwa akimsaidia kuuza nguo kwenye duka lake. Mwaka 2017, video ya Nipsey akiwa na baba yake pamoja na kaka yake wakiuza nguo kwenye duka lake la ‘Marathon’ ilikuwa maarufu ikisambazwa na mashabiki wake.

Ingawa alikuwa mtukutu, alimpenda sana mama yake, aliwahi kusema kuwa wakati baba yake alipenda kuangalia CNN, mama yake alikuwa akimbana aende chumbani akajisomee.

“Mimi nawashauri, ukiweza kaa nyumbani kwa mama yako hata ukiwa mkubwa na tunza pesa zako kwa ajili ya kazi na biashara,” alisema Nipsey.

Nipsey Hussle akiwa na baba na kaka zake, Eritrea 2018

Kifo chake kimewaumiza wengi Eritrea. Nchi imegubikwa na majonzi. Ni mwaka jana tu, Nipsey Hussle aliitembelea nchi hiyo akiwa na baba yake pamoja na kaka yake.

Yapo mengi aliyoyafanya yaliyozua utata mkubwa. Mojawapo ni pale alipotangaza kuwa anataka kuachia makala maalum ya ‘Dkt. Sebi’, mtaalam wa tiba ambaye anadaiwa kuingia matatani dhidi ya Serikali ya Marekani baada ya kudai kuwa amegundua dawa ya kutibu Ugonjwa wa Ukimwi/Virusi vya Ukimwi.

Huo ni sehemu ya mradi tata aliokuwa ameuahidi kabla ya kifo chake. Muigizaji/mtangazaji Nick Cannon yeye ameahidi kuubeba msalaba huo na kuendeleza juhudi za kuachia makala hiyo inayodaiwa kufichua mengi kuhusu sakaka la Dkt. Sebi ambaye jina lake halisi ni Alfredo Darrington, mzee aliyezaliwa mwaka 1933.

Mungu ampumzishe kwa amani Nipsey Hussle, ametuachia hazina ya muziki na kulitangaza vizuri jina la Eritrea na Afrika kwa ujumla.

 

Pierre amuibua Fatma Karume, 'Kila mtu ana haki ya kuishi atakavyo'
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Aprili 5, 2019