Na Kika:

Mradi wa kuzalisha umeme kwenye bonde la mto Rufiji umekuwa ukipingwa vikali na mataifa yaliyoendelea. Wanaharakati wanaojiita watetezi wa mazingira wamekuwa wakiupinga mradi huo, wakisema utakuwa na athari kubwa kwa viumbe na hata kukausha maji mengi ya mto huo.

Mradi huo unatajwa kuwa unatokana na maono ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyetamani taifa la Tanzania lijitosheleze kwa nishati ya umeme, ambapo kati ya mwaka 1976 mpaka 1980, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Norway, kupitia Kampuni ya Norplan & Hafslud, zilifanya upembuzi yakinifu (feasibility study), na kubaini kuwa, Mradi huu wa Bonde la Mto Rufiji una uwezo wa kuzalisha umeme Megawati 2,100. Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali, ikiwemo matatizo ya kifedha, Mwalimu Nyerere hakuweza kuutekeleza.

Sasa, Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeutangazia ulimwengu kwamba itauendeleza mradi huo utakao gharimu Dola za Marekani bilioni 2.9, sawa na takriban shilingi za Tanzania trilioni 6.558, huku ikikataa katakata vitisho vya wanaharakati wa mataifa ya Ulaya kwamba mradi huo utasabisha athari kwa mazingira.

Kampuni ya M/S Arab Contractors kutoka Misri ndiyo iliyoshinda zabuni ya mradi huu na mnamo Desemba 12, 2018 Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli pamoja na mgeni wake Dkt. Mostafa Madbouly, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri waliongoza hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji mradi huo.

“Tulitumia vigezo vikubwa vinne: yaani uhakika wa chanzo chenyewe; gharama za utekelezaji (investment cost); gharama za uzalishaji (cost of generation); pamoja na tija au manufaa yanayotarajiwa kupatikana; tulibaini kuwa Mradi huu ndio unaifaa zaidi nchi yetu kwa sasa.” Sauti ya Rais Magufuli ya kujiamini ilisikika katika hafla ya kusaini mkataba huo.

Ikiwa mradi huu utakamilika, utakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2,100 na hivyo kupunguza mahitaji makubwa ya umeme hapa nchini.

Hivi karibuni Askofu Gwajima alimtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli huko Ikulu, dhamira yake ilikuwa ni kumpongeza kwa kuthubutu kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo huo wa kuzalisha umeme kwenye bonde la mto Rufiji.

Askofu Gwajima amesema hakuna haja kwa serikali ya Tanzania kuogopa kutekeleza mradi huo kwa kuogopa kelele zisizo na msingi za mataifa ya Ulaya. Ameendelea kueleza kuwa sisi kama watanzania ni lazima tuwe na vipaumbele vyetu katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye maslahi kwa wananchi pasipo kujali matakwa ya mataifa ya Ulaya.

Kuna kila sababu ya kuamini kwamba agenda ya uchafuzi wa mazingira inayotajwa na wanaharakati wa mataifa ya Ulaya siyo ya kweli. Ni dhahiri kuna hofu kubwa ya mataifa ya Ulaya wanayoiona, kwani Tanzania itakuwa imejikomboa kiuchumi kwa kiasi kikubwa kwa kuwa na umeme wa kutosha.

Mradi huo, katika hali halisi kabisa, utasaidia kutunza mazingira ya nchi. Kwanza, kwa sababu, umeme wa maji ni rafiki wa mazingira. Pili, eneo litakalotumika kuutekeleza ni dogo; litakuwa kati ya asilimia 1.8 hadi asilimia 2 ya eneo zima la Hifadhi ya Selous, ambalo ni kubwa kuliko baadhi ya nchi. Sababu ya tatu ni kwamba, Mradi huu utapunguza ukataji miti nchini.

Gharama za umeme zimekuwa ni ghali mno kwa matumizi ya kawaida kwa watanzania na hata kwa wawekezaji. Taarifa zinaonesha kuwa wakati bei ya umeme ikiuzwa kwa fedha za Marekani kwa st. 0.12 huko Ulaya, hapa nchini umeme huo huuzwa kwa st. 11 – 12 (kwa unit).

Serikali ya awamu ya tano ina miradi mikubwa inayoitekeleza. Kuna mradi mkubwa wa kukarabati reli itakayokuwa ikisafirisha treni ya kisasa inayotumia umeme. Reli hiyo tayari imeshaanza kukarabatiwa na inaanzia Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora hadi Kigoma, hali kadhalika reli hiyo itakarabatiwa kuelekea Shinyanga hadi Mwanza.

Kuna neema kubwa inakuja baada ya kukamilika kwa ukarabati wa reli hiyo. Taarifa zinaeleza kwamba abiria watakaokuwa wakisafiri kwa treni hiyo watakuwa wakitumia muda wa saa nane tu hadi kufika mkoani Kigoma ama Mwanza. Kwa usafiri wa sasa kwa kutumia treni ya kawaida, abiria hutumia saa 72 ama zaidi. Treni hiyo ya kisasa itakuwa ikisafirisha mizigo mingi na mikubwa zaidi ya sasa inavyosafirishwa na magari makubwa.

Siyo hivyo tu kwamba treni hiyo ya kisasa itatoa unafuu wa kusafirisha mizigo mikubwa, pia itasaidia kupunguza uharibifu wa barabara zinazoelekea mikoani unaosababishwa na magari makubwa ya mizigo.

Hivyo, hiyo yote ni ishara kwamba uchumi wa viwanda ambao umelengwa kufikiwa na serikali ya awamu ya tano, hautaweza kufikiwa endapo hakutakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika.

Maendeleo ya Tanzania yanawahitaji wawekezaji wa ndani na wale wa kutoka nchi za nje. Serikali inaona waziwazi kwamba ili kuweza kuwavutia wawekezaji ni lazima iwasaidie kwa kuwaandalia umeme wa kutosha na wenye gharama nafuu. Kuwapata wawekezaji wengi ni faida kwa ukuaji wa uchumi wa nchi hii, kwani wawekezaji hao watakuwa na uwezo wa kulipa kodi na hali kadhalika kutakuwa na nafasi nyingi za ajira kwa watanzania.

Kuutekeleza mradi kuzalisha umeme kwenye bonde la mto Rufiji kuna tafsiri tatu; Tafsiri ya kwanza ni kwamba serikali ya awamu ya tano inayaenzi, kuyaheshimu maono ya mbali ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere dhidi ya ustawi wa wananchi wake.

Tafsiri ya pili ni ujasiri, uthubutu, kujiamini kwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli katika kusimamia maslahi ya wananchi wake. Ameweza kutupilia mbali njama za mataifa ya kinyonyaji na kibeberu ya mataifa ya Ulaya Magharibi.

Msimamo huo wa kutokuyumba unafananishwa na msimamo wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipoyakataa masharti magumu ya Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Baadhi ya masharti yaliyokataliwa na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kukataa kubinafsisha au kuuza mashirika ya umma, uchangiaji kwenye sekta za elimu, afya na nyinginezo pamoja na sera zote za kinyonyaji na kibeberu za mataifa ya Ulaya Magharibi kama vile Marekani, Uingereza na washirika wake.

Tafsiri ya tatu ni ndoto ya serikali ya awamu ya tano kutaka kuliona taifa hili linakuwa ni mojawapo ya mataifa hapa duniani, ambapo uchumi wake utakuwa unakua kwa kasi sana.

Jarida moja la mambo ya Uchumi (Fox) limetoa taarifa yake kuhusiana na kukua kwa uchumi hapa nchini. Jarida hilo limeutaja mradi huo wa kuzalisha umeme kwenye bonde la mto Rufiji kuwa mojawapo ya miradi mikubwa ambayo itaipaisha kimaendeleo na kiuchumi serikali ya Tanzania.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 22, 2019
Ellipsis Digital kutoa mafunzo ya utengenezaji wa programu za kompyuta bure