Na: Shaban Kondo

Mtunisha Misuli na bingwa wa dunia wa kunyanyua vitu vizito, Mmarekani Ronnie Coleman amewahi kukaririwa akisema, “kama unaendelea kufanya ulichokuwa unafanya kwa mtindo uleule basi tarajia kuwa utafika palepale ulipokuwa unafika siku zote.” Coleman akiwa na kilo 135 aliweka juhudi na akaweza kunyanyua kilogram 410.

Aliyekuwa bingwa wa dunia wa masumbwi ambaye hajawahi kupigwa, Floyd Mayweather ambaye ana ukwasi usio kifani amewahi kusema, “Watu wanapoona nilichonacho sasa, hawawezi kupata picha ya nilikotoka.”

Mbwana Ally Samatta, kijana aliyeweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza na Timu ya Ulaya na kuifunga na sasa kusajiliwa na timu ya Ulaya kwa Pauni milioni 10, wanaomuona leo hawawezi kupata picha ya jinsi alivyoanza kutandaza soka mitaani; lakini kwakuwa hakuwa anafanya yaleyale kila siku leo amepata matokeo tofauti na ameiweka Tanzania kwenye ‘Ligi ya Dhahabu’.

Januari 2020 utaendelea kuwa kwenye kumbukumbu za wadau wa soka nchini Tanzania, kufuatia taarifa iliyomuhusisha nahodha na mshambuliaji wa timu yao Taifa Stars, Mbwana Ally Pazi Samatta; ni baada ya mchezaji huyo kusajiliwa na mabingwa wa barani Ulaya mwaka 1981–82 Aston Villa, akitokea KRC Genk kwa gharama inayotajwa kufikia Pauni milioni 10.

Aston Villa walifanikisha lengo la kusajili kijana huyo wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 27, baada ya kumfuatilia kwa mapana na marefu akiwa nchini Ubelgiji ambapo aliisaidia klabu ya KRC Genk kutwaa ubingwa wa msimu wa 2018/19.

Katika kipindi chote alichoitumikia klabu ya KRC Genk ambayo ilimsajili akitokea TP Mazembe ya DR Congo, Samatta alifanikiwa kufunga mabao 43 katika michezo 101 aliyochezwa tangu mwaka 2016.

Mbali na watanzania kuwa na furaha ya kuona Mbwana Samatta akifanikisha ndoto za kucheza soka lake nchini England, baba mzaa chema, Mzee Ally Pazi Samatta yeye alidondosha chozi la furaha na kujipa raha kwa namna yake.

Mzee Samatta ambaye ni mstaafu wa jeshi la polisi, amesema alimwaga machozi ya furaha Januari 20, baada ya kuthibitishiwa na mtoto wake kuwa amekamilisha dili la kujiunga na Aston Villa.

Mbali na kumwaga machozi mzee huyu ambaye aliwahi kucheza soka nafasi ya ulinzi wa lango (goal keeper), alisema muda wa usiku kucha aliutumia kucheza muziki wa zamani ikiwa ni sehemu ya furaha ya kusikia kweli mwanae amekamiliha ndoto za kucheza soka katika ligi ya England ambayo tangu akiwa mdogo alitamani kucheza.

Waswahili husema, ‘Mhunzi ndiye ajuaye yalikotoka makali ya mkuki wake’. Mzee Samatta ameeleza yalikotoka makali ya mwanaye, akinolewa na kujinoa tangu mtaani na kisha kujiunga na klabu ya Mbagala Market ambayo baadae ilinunuliwa na Tajiri Mohamed Dewji na kubadilishwa jina kutoka Mbagala Market na kuitwa African Lyon.

Kumbukumbu zinaonyesha mshambuliaji huyo aliitumikia African Lyon kuanzia mwaka 2008-2010.

Nyota iliyoonekana asubuhi iliendelea kung’aa, mabingwa wa soka Tanzania bara kwa sasa Wekundu Wa MSimbazi, Simba SC walimnyakua.

Hata hivyo, Samatta hakuwa na muda mrefu ndani ya klabu hiyo, kwani alicheza msimu mmoja wa 2010–2011 lakini aliacha fadhila ya kupachika mabao kumi na tatu (13) kwenye michezo 25 aliyocheza.

Wachezaji wa timu ya Simba kutoka kushoto,Rashid Gumbo,(aliyeficha sura), Mbwana Samata na Juma Jabu,wakishangilia baada ya Samata kufunga bao dhidi ya timu ya Elan Club ya Comoro wakati wa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam. Simba ilishinda mabao 4-2. (Picha na Yusuf Badi).

Rapa Fid Q na Mzee Zahir Zorro kwenye wimbo wao ‘Ripoti za Mtaa’, alisema “kizuri ni kizuri lakini chenye ubora ni bora.” Ubora wa Samatta ulianza kumpa mng’ao wa haraka mbele ya wachezaji wengi wazuri.

Mwaka 2010 wakati wa mchezo wa mkondo wa pili wa ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya Simba dhidi ya TP Mazembe, Mbwana alifunga bao la kufutia machozi na kuufanya mpambano huo uliounguruma uwanja wa Taifa Dar es salaam kumalizika kwa wenyeji kukubali kichapo cha 3-1 na kutupwa nje ya michuano hiyo.

Bao alilofunga Samatta na ubora aliouonesha kati ya wachezaji wazuri ndio ilikua chachu kwa viongozi wa TP Mazembe kuvutiwa naye. Bilas haka walipokuwa njiani walikumbuka alipowapa wakati mgumu. Baada ya muda waliamua kutuma ofa ya kumsajili, na Simba SC wakafungua mlango, wakakubali dili hilo.

Hapo ndipo Samatta alipoonyesha sehemu ya kuanza safari yake kikamilifu katika ukanda wa soka la kimataifa. Alipambana vilivyo katika ligi ya DR Congo pamoja na kwenye michezo ya kimataifa. Kwa juhudi zake, alifanikiwa kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2015.

Nambari hazidanganyi, rekodi zake zilijiandika kwa kalamu pana (bold), na kila mmoja aliziona. Akiwa TP Mazembe alicheza michezo 103 na kufunga mabao 60.

Januari 2016 Mbwana alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani ya Afrika, hatua ambayo iliendelea kudhihirisha namna gani kijana huyu alikua amejidhatiti kutimiza lengo lake la kucheza soka la ushindani zaidi duniani.

Katika kinyang’anyiro hicho, Mbwana aliibuka kidedea kwa kujizolea alama 127, akimshinda aliyekua mlinda mlango wa TP Mazembe Robert Kidiaba aliepata alama 88 na Baghdad Bounedjah kutoka Algeria akishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 63.

Agosti mwaka huo, milango mingine mikubwa nje ya bara hili ilifunguliwa kumkaribisha ‘Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani’, Samatta. Alijiunga na Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji ambayo aliitumikia katika michezo 101 na kufunga zaidi ya mabao 60.

Akiwa na klabu hiyo Mbwana alicheza michuano ya Europa League na msimu huu wa 2019/20 alicheza ligi ya mabingwa barani Ulaya, na kuifunga Liverpool ambayo kwa sasa ndio kigogo kizito katika ligi ya England.

Akiwa na KRC Genk ametwaa ubingwa Wa Ubelgiji (Belgian Pro League) msimu wa 2018–19, na pia alitwaa ubingwa wa Belgian Super Cup mwaka 2019.

Hadi tunaandaa makala hii, Mbwana bado hajaanza kucheza Ligi ya England akiwa na klabu yake mpya ya Aston Villa, lakni huenda mwishoni mwa juma hili akaonekana akiwa na jezi yake namba 20, pale The Villians watakapopambana dhidi ya AFC Bournemouth, mnamo Februari Mosi.

 

Mafanikio mengine ambayo Samatta ameyapata katika safari yake ya soka ni:

-Kutwaa ubingwa wa DR Congo (Linafoot) mwaka 2011, 2012, 2013 na 2014.

Ubingwa DR Congo Super Cup: mwaka 2013, 2014

-Ligi ya mabingwa barani Afrika (CAF Champions League) mwaka 2015.

Tuzo na mafanikio binafsi.

  • Amewahi kuingia kwenye kikosi bora cha Bara la Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za bara hilo (African Inter-Club Player of the Year) mwaka 2015.
  • Amewahi kuingia kwenye kikosi bora cha bara la Afrika (CAF Team of the Year) mwaka 2015.
  • Alikua mfungaji bora wa ligi ya mabingwa barani Afrika (CAF Champions League top scorer) mwaka 2015.
  • Alitwaa tuzo ya Ebony Shoe mwaka 2019.
  • Aliwahi kutwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu (Belgian First Division A Golden Shoe) baada ya kuibuka mfungaji bora msimu wa 2018–19.

Huyo ndiye Mbwana Ally Samatta.

Moja kati ya siri za mafanikio ya Samatta ni nidhamu na kujituma, pamoja na unyenyekevu. Hii tutaizungumza kwa undani siku nyingine. Kwa sasa tusubiri tuone anavyozichapa Manchester United, Manchester City, Chelsea na wababe wengine.

 

Polisi wakana kumkamata mwanafunzi wa UDOM
Video: Rais Magufuli "Lugola nakupenda lakini kwa hili hapana"