Rafiki yangu Mwita, tuliyeishi wote katika kijiji cha Nyanchabhakenye mkoani Mara aliwahi kunitoa chozi aliponisimulia jinsi ambavyo kaka yake mpendwa akiwa na familia yake walivyopoteza maisha kwa ajali mbaya ya gari mwishoni mwa mwaka 2017.

Kwa bahati mbaya, wakati huo ananisimulia tulikuwa tunasafiri wote kwa gari binafsi na tulipita katika eneo ambalo lilikuwa na kona ya kawaida tu lakini tulishuhudia ajali mbaya ya gari dogo lililogongana uso kwa uso na gari la mafuta. Ni ajali hiyo ndiyo iliyovuta kumbukumbu mbaya ya kifo cha kaka yake na aliamua kunishirikisha undani wa simulizi ya majonzi baada ya kunyamaza kimya kwa takribani sekunde 30 akisitisha mjadala tuliokuwa tunaendelea nao kuhusu nafasi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika siasa za Tanzania kwa mazingira yaliyopo.

Alisema kaka yake alikuwa amepata kazi nzuri mwezi mmoja uliopita katika kampuni kubwa ya Gesi iliyoko maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam, na aliamua kuwakusanya ndugu zake nyumbani kwao ili waweze kusherehekea kwa pamoja sikukuu ya Mwaka mpya na kumshukuru Mungu kwa mafanikio. Wakiwa wamejikusanya wakimsubiri nyumbani kwa hamu, tayari wameshafanya maandalizi ya sherehe, wakinunua vyakula na vinywaji na kupiga muziki wakati wote, walipigwa na ubaridi mzito ghafla walipopata taarifa kuwa ndugu yao na familia yake walipata ajali mbaya baada ya kugongana uso kwa uso na basi la abiria.

Alisema basi lilikuwa kwenye mwendo mkali sehemu ya kona na katika hali isiyo ya kawaida lililazimisha kulipita (kuovertake) gari lingine dogo wakati mbele yake kuna gari (la kaka yake Mwita) likiwa linapishana na magari hayo.

Taarifa ya ajali hiyo iliwafanya wapate ubaridi mithiri ya watu waliolowekwa kwenye barafu kali. Sherehe iligeuka msiba katika kijiji cha Nyanchabhakenye.

Lakini baada ya tafakuri ya muda mrefu, ndugu na hasa baba mzazi wa marehemu pamoja na marafiki wa karibu waliamini kuwa ajali ile sio ya kawaida bali ni ‘kafara za wenye magari na kutupiwa mapepo ya mwisho wa mwaka’. Kadhalika, wengi waliamini kuwa alitupiwa mapepo mabaya kutokana na wivu dhidi ya mandeleo yake ya kikazi.

Ajali iliyowahi kutokea nchini

Simulizi hilo la majonzi lilinishtua, nilitamani kuyajua mapepo hayo yanayosababisha ajali hasa mwisho wa mwaka; na ndipo nilipoanza udadisi kwa kufanya utafiti mdogo.

Kwa mujibu wa ripoti ya usalama barabarani, kati ya mwaka 2016 na 2017, idadi kubwa ya ajali iliripotiwa katika kipindi cha mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka. Yaani kati ya Desemba 2015 hadi Machi 2016 pekee hapa nchini jumla ya ajali za barabarani 2,443 ziliripotiwa na katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2016/17 takribani ajali 1,447 ziliripotiwa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kuwa mbali na idadi kubwa ya majeruhi, takribani watu milioni moja na laki mbili (1,200,000) hufariki kwa ajali za barabarani kila mwaka duniani kote. Shirika hilo limeenda mbali na kueleza kuwa karibu watu watatu kati ya watu 10,000 hufariki duniani kwa ajali za barabarani. Ripoti hiyo imeongeza kuwa ajali za barabarani ni sababu kuu ya majeraha na ulemavu usio wa asili duniani.

Kwa bahati mbaya, Tanzania ilitajwa kushika nafasi ya pili kati ya nchi tano za Afrika Mashariki kwa kuwa na idadi kubwa ya ajali za barabarani ikiwa nyuma ya Uganda. Kwa picha ya juu zaidi ya bara la Afrika, ripoti hiyo inaeleza kuwa takribani watu 24,000 kwa kila watu 100,000 hupoteza maisha kwa ajali za barabarani.

Kwa kuzingatia hilo, katika nchi nyingi barani Afrika, idadi kubwa zaidi inaonekana katika kipindi cha mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka ikihusisha vyombo vya moto na waenda kwa miguu pia.

Udadisi wangu wa kuyafahamu mapepo yanayoleta ajali hizi ulianza kwa kuyasaka mapepo kwenye ripoti rasmi, nikianza na sababu za ajali barabarani, ndipo nilipogundua kuwa pepo kuu linalosababisha ajali za barabarani ni pepo la uzembe.

Ripoti ya Kikosi cha Usalama Barabarani nchini inaonesha kuwa katika kipindi cha mwisho na mwanzo  wa mwaka mpya, mwaka 2015/2016 kati ya ajali 2,443, uzembe uliongoza ukisababisha ajali 1,287 kwa ujumla kutoka kwa madereva wa vyombo vya moto na waenda kwa miguu. Hii ni zaidi ya nusu ya ajali zote zilizotokea.

Vivyo hivyo, kwa kipindi cha mwisho wa mwaka 2016 na mwanzo wa mwaka 2017, uzembe umetajwa kama chanzo cha ajali 891 ambazo ni karibu robo tatu ya ajali zote katika kipindi hicho.

Hata hivyo, pepo hili halifanyi kazi peke yake, linasaidiana kwa ukaribu na pepo la tamaa na pepo la haraka zisizojali.

Kwakuwa kila mtu anatamani kusafiri akale sikukuu na familia yake, idadi kubwa ya abiria inayozidi huduma za usafiri huyasogeza karibu mapepo haya. Pepo la tamaa ya fedha huwavaa madereva na wamiliki wa magari ambao wanajikuta wakijaza abiria na mizigo kupita kiasi, kuendesha mwendo kasi zaidi pasiporuhusiwa ili wafanye safari nyingi zaidi pamoja na kupuuzia kufanya matengenezo ya kutosha wakihofia kupoteza muda wa kutengeneza pesa njiani.

Kadhalika, pepo la haraka zisizojali usalama huwakumba baadhi ya abiria waliofurika kwenye vituo vikuu vya mabasi. Abiria hao hujikuta wakiwaza kufika waendapo bila kujali hali ya chombo walichopanda na namna kilivyojaza kupita kiasi. Wanajifumba macho na kuziba ufahamu kuwa chombo chochote cha moto kimetengenezwa kwa idadi kamili ya watu na uzito wa mizigo ili kimudu safari husika kwa usalama.

Katika kutokomeza mapepo haya, Serikali mbali na kutumia hatua za kisheria na kitaalum imekuwa ikishirikisha pia imani kwa kuyaombea mabarabara na vyombo vya usafiri, wakiyakemea mapepo haya.

Mwezi Juni mwaka huu, kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa ajali za barabarani mkoani Mbeya, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla aliwaongoza wananchi wa mkoa huo kufanya ibada maalum za dini zote ikiwa ni pamoa na za kimila kukemea mapepo ya ajali. Hali hiyo ilitokana na kuripotiwa kwa vifo vya watu 45 vya ajali barabarani ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tu.

“Tunatekeleza sheria na maagizo yote tunayopewa na viongozi wetu wa kitaifa, lakini busara zinatuelekeza kumrudia Mungu. Hivyo, tunaomba siku ya Alhamisi wananchi wote, dini zote na makabila yote, tukutane kumuomba atuepushie matatizo haya mkoa wetu uwe shwari,” alisema Makalla.

Baadhi ya Machifu wa Mbeya wakitembea kufanya maombi dhidi ya ajali za barabarani

Vikosi vya usalama barabarani vimefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa ajali za barabarani zinapungua ambapo taarifa rasmi ya Kikosi cha Usalama Barabarani nchini imeeleza kuwa ajali hizo zimepungua kwa zaidi ya asilimia 40 kutokana na hatua zinazochukuliwa. Lakini bado kuna ishara za hatari katika kipindi hiki.

Chukua hatua, kemea mapepo haya kwa vitendo. Ni bora kuchelewa lakini ufike salama. Kuwa askari wa usalama wako, mkatae dereva anayejaribu kukuwahisha bila kufuata utaratibu kwani huyo amekaribisha mapepo hivyo yakemee bila simile.

Askari wa usalama barabarani akiwa kazini 

Usiogope tochi ya polisi barabarani, muogope kama ukoma dereva anayekimbia bila kuzingatia alama za barabarani.

Usikubali msemo wa ‘tochi za polisi zimezidi’, kumbuka ‘ajali zinazidi tochi za polisi’. Fika salama hata ikiwa ni kwa kuchelewa uyakwepe mapepo mabaya.

Video: Magufuli amlipua waziri wake, Vigogo waliouza meli 10 sasa maji ya shingo
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 22, 2018

Comments

comments