Na Ghati:

Wazee wenye hekima walioishi enzi hizo (wahenga) walisema, “aliyejaribu kuking’oa kisiki, ndiye aijuaye siri ya maumivu ya mkono.” Lakini ni haohao waliosema, “maji yaliyochemka yakapoa, yakichemka tena hupungua ujazo.”

Misemo hii itunze vyema, itakupa picha pana kabla ya kuhitimisha makala hii inayotokana na joto la utabiri wa jina la mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Hadi mwaka 2017, miaka miwili baada ya uchaguzi mkuu, hakukuwa na shaka kuwa  Chadema, pamoja na kuwa na wanasiasa machachari kama chama kikuu cha upinzani, endapo uchaguzi mkuu ungeitishwa katika kipindi hicho jina la waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa lingekuwa na asilimia 95 ya kupitishwa kuwania tena nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hii inatokana na mtaji mkubwa pamoja na faida ya kihistoria ya ongezeko la wabunge waliyoipata mwaka 2015, baada ya kumsimamisha Lowassa aliyekuwa mbunge wa Monduli kwa miaka 20, kuwania nafasi hiyo muda mfupi baada ya kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mtaji wa kura 6,072,848   (sawa na 39.97%) kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na wabunge 34 wa Chadema wa kuchaguliwa, kutoka 20 wa mwaka 2010. Kwa ujumla aliwapa Ukawa wabunge 116. Mtaji huu uliandika historia; na huenda ulijibu swali la aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Wilbroad Slaa aliyeuliza swali la mtego kabla ya kumpokea, “Lowassa ni asset au liability (ni mtaji au dhima/mzigo)?” Lakini kwa sasa mjadala usio na majibu ya pamoja ni kuhusu mtaji huo wa Lowassa kuwa umeshuka, umepanda, uko palepale au amefilisika?

Hata hivyo, hali ilianza kuonekana tofauti hasa miezi ya mwisho ya mwaka jana, baada ya jina la mwanasiasa machachari, Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema kuanza kutajwa kwenye mitandao ya kijamii kama jina lenye nafasi ya kuwania Urais kupitia Chadema mwaka 2020.

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akimsalimia Tundu Lissu (Mb), alipoenda kumjulia  hali hospitalini Jijini Nairobi nchini Kenya baada ya kupigwa risasi

Kwanini Lissu:

“Jogoo anayewika sana bandani huwa wa kwanza kuhesabiwa.” Kwa ufupi msemo huu unatoa picha ya awali ya kwanza, kwanini Lissu anatajwa.

Tutakubaliana kuwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Lissu ndiye mpinzani aliyeongoza kwa kuzungumza mambo mengi akiikosoa Serikali hata pale ilipofanya mambo ambayo kiuhalisia wengi waliona yanafaa kupongezwa. Lissu aliziita pongezi hizo kwa Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni ‘vigelegele vya msimu’.

Kwa bahati, alipata kofia nyingi zilizomuwezesha kuzungumza mara kwa mara kwa namna tofauti. Kwanza, kama Mbunge wa Singida Mashariki. Pili, kama Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni. Tatu, kama mwanasheria wa Chadema. Nne, kama Rais wa Chama Cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS). Tano, kama wakili aliyetetea kesi maarufu hasa za watu wenye mlengo wa upinzani.

Kofia hizi zote zilimpa nafasi ya kusema mara nyingi, japo alipenda pia kutumia kofia ya sita ya “mimi hapa nasema kama mwananchi mwenye haki ya kuhoji haya yote.”

Ingawa wanasema ni vigumu kumtofautisha mwanasiasa hasa mpinzani na mwanaharakati, Lissu ni mwanaharakati zaidi kuliko mwanasiasa.

Tukio la kushambuliwa kwa risasi takribani 25 na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 katika eneo la Area D jijini Dodoma, akitokea Bungeni, lilifanya jina la Lissu kutajwa mara nyingi zaidi. Na hata ambao walikuwa hawamjui walipata nafasi ya kujua angalau jina tu la ‘mwanasiasa wa Chadema aliyejeruhiwa kwa risasi lukuki’.

Shukurani kwa Mungu, leo Lissu ni mzima baada ya kupata matibabu katika hospitali tatu tofauti ambazo ni Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi Kenya na mwisho nchini Ubelgiji, akifanyiwa upasuaji katika sehemu nyingi za mwili wake. Siku yoyote kuanzia leo, anaweza kurejea nyumbani anakosubiriwa kwa hamu na wafuasi wake, familia pamoja na ndugu na jamaa.

Ni wakati huu ambapo ameendelea kutumia nafasi ya sikio alilopewa na umma, kama alivyodai kuwa ‘mgonjwa wa Taifa’, kupiga kelele ambazo wakati mwingine zina ‘ukakasi dhidi Serikali’.

Kutokana na kelele hizo, amekuwa jogoo wa kwanza kuhesabiwa bandani, na hesabu hizi zilianza kufanywa na wafuasi wa upinzani kupitia mtandao wa Twitter na kufanya wazo hilo kuwa maarufu hadi kushika masikio ya vyombo vya habari vya kimataifa kama BBC.

Lissu anatambua nguvu ya Lowassa

Kwenye mahojiano na BBC, ingawa Lissu alionesha kuwa na utayari wa kugombea nafasi ya urais endapo Chadema watampa jukumu hilo, bado anaamini anamhitaji Lowassa kuongeza nguvu.

“Hapana cha mpambano [kati yangu na Lowassa], kama chama changu kitasema ‘Mzee Lowassa hebu muachie huyu kijana apambane, haya mapambano ya sasa ni makali kidogo yanahitaji nguvu zaidi, hebu msaidie huyu kijana kwenye hili jukumu’… chochote kinawezekana,” alisema Lissu.

Ikumbukwe pia kuwa nguvu ya Lissu ilitumika sana kumnadi Lowassa kwenye uchaguzi wa mwaka 2015. Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete alitumia muda wake kujibu hoja za Lissu kuhusu sakata la Richmond ambalo Lissu alilihamisha kwa hoja kutoka kwa Lowassa na kuitwisha Serikali ya Dkt. Kikwete.

Tofauti ya Lissu na Lowassa kisiasa

Hawa ni watu wawili tofauti sana kwenye ulingo wa Siasa. Hakuna wanachofanana zaidi ya kuendana kiitikadi wakiwa wote ni wafuasi wa chama cha upinzani.

Lissu ni mwanaharakati zaidi ya mwanasiasa, anayeamini katika ‘kupiga kelele’ zaidi na kuleta vuguvugu. Lakini Lowassa ni mwanasiasa zaidi ya mwanaharakati. Yeye ni mtaalam wa mbinu za chini kwa chini zenye maneno kiasi yanayozingatia sana mstari wa upande wa pili.

Lowassa sio wa siasa za majukwaani na mitandaoni. Ndio sababu dakika 5 hadi 15 zilikuwa zinamtosha akiwa jukwaani kuelezea kipaumbele chake cha ‘Elimu… Elimu… Elimu‘ kwenye uchaguzi mkuu, na bado akawashawishi wapiga kura milioni 6. Lowassa hapendi purukushani na kunyoosheana vidole hadharani kwenye siasa na ndio sababu hupata heshima hata kutoka upande wa pili (CCM).

“Lowassa ni muungwana,” alisema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Omari Kinana baada ya uchaguzi wa mwaka 2015. Sifa hizo zenye mfanano na hizo na zaidi amekuwa akipewa hadharani na Rais John Magufuli.

Edward Lowassa na Abdulrahman Kinana wakibadilishana mawazo, Agosti 2016 jijini Dar es Salaam

Hata hivyo, ni sifa hizo anazopewa na Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM zinazompunguzia alama muhimu kwa baadhi ya wafuasi wa upinzani.

Lowassa ni mvumilivu hata anaposhambuliwa vikali. Amewahi kushambuliwa vikali na upinzani akiwa CCM na kuonekana kama kinara wa hoja ya ufisadi ya Chadema. Lakini pia alipohamia Chadema, CCM walimrushia kila aina ya kombora ili mradi tu wamjeruhi kisiasa. Lakini mwanasiasa huyu hutulia, huvumilia na husubiri nafasi yake nzuri na kurusha mshale wake panapotakiwa. Huchagua maneno ya kupinga jambo na hukwepa mikwaruzano na dola.

“Naomba msinigombanishe na Rais, naomba tumuache afanye kazi zake vizuri kwa mujibu wa Katiba,” ni baadhi ya maneno ya Lowassa, ambaye alizua taharuki kwa baadhi ya wafuasi wa Chadema alipokutana na Rais Magufuli Ikulu bila kuwataarifa viongozi wa chama hicho.

Huenda hali hii kwa wapinzani wengi, inaweza kuwa ni sifa hasi dhidi ya Lowassa kwenye siasa za upinzani zilizozoeleka.

Kwa mfano, Lissu ni miongoni mwa waliopinga vikali mkutano wa Rais Magufuli na Lowassa tena bila viongozi wa Chadema kufahamu. Alienda mbali na kupinga sifa alizoonekana anazitoa Lowassa kwenye video iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ambayo hata hivyo Lowassa alisema ilieditiwa baadhi ya mambo aliyoyajengea hoja.

“Viongozi na wanachama wetu wanashambuliwa hadharani kwa mapanga na hata kwa risasi, kumsifia Rais ni kumuunga mkono yeye. Katika mazingira ya kesi nyingi za kutunga dhidi yetu, ‘kazi nzuri’ inayofanywa ina maana gani, kama sio kuhalalisha ukandamizaji tunaofanyiwa. Kwa vyovyote vile, kitendo cha Lowassa sio cha kunyamaziwa au kuhalalishwa kwa hoja nyepesi nyepesi.” Alisema. Lissu kupitia waraka wake akiwa Ubelgiji anapotibiwa.

Lissu ni mwanasiasa kijana, mzuri wa kujenga hoja, kuzielezea kwa undani na kushawishi kwa nguvu ya hoja hadi kuwaaminisha wasio amini. Uvumilivu kwake ni fumbo la imani! Mishale yake haina subira na huipaka sumu ya kutosha hata kama mnyama anayemtaka ni mdogo zaidi ya panya.

Je, unaweza kusema dhahiri kuwa kauli ile iliyosemwa na Lowassa hapo juu kuhusu Rais inaweza kuwa ya Lissu unayemfahamu? Abadan!

*Katika siasa, Lowassa mbali na uzoefu wake, ana mtaji mkubwa. Ukimya wake haujawahi kuwa chanzo cha kuwapoteza wafuasi wake, kwa kuzingatia historia. Kwa mfano, tangu mwaka 2008 alipojiuzulu Uwaziri Mkuu alikuwa kimya na alizungumza mara chache sana bungeni. Lakini mwaka 2015 kishindo cha ukimya wake kilileta mtetemo mzito kwenye siasa za Tanzania.

Pia, kwakuwa amewahi kujaribu kuking’oa kisiki (CCM), yeye ndiye ajuaye siri ya maumivu ya mikono yake, kama wasemavyo wahenga. Hivyo, anajua mizizi ya kisiki husika ilipo.

Na ingawa wanasema CCM ya sasa sio ile ya zamani, bado naamini ‘Jasiri haachi asili’. Hivyo, bado Lowassa anaijua CCM kiasi fulani.

Bado naamini, kuhusu mtaji wa kisiasa alionao Lissu kwa sasa, inaweza kuwa pungufu au sawa na mtaji aliokuwa nao Dkt. Wilbroad Slaa hadi 2015 akiwa ndani ya Chadema. Mtaji ambao Lowassa alionesha kuuzidi mara tatu akiongezewa nguvu na ushirikiano wa vyama vya siasa.

Edward Lowassa akiwa kwenye mkutano wa kampeni 2020

Nimemtaja Dkt. Slaa kwa sababu mtindo anaoutumia Lissu leo una mfanano mkubwa na ule wa Dkt. Slaa, yule aliyekuwa na orodha ya aliodai ni mafisadi.

Lakini Lissu anayo nafasi dhidi ya Lowassa kama tutautumia msemo wa wahenga kuwa, “maji yaliyochemka yakapoa, yakichemka tena hupungua ujazo.” Yaani kwakuwa Lowassa alishaleta vuguvugu, anaweza asilete matokeo kama yale akijaribu tena.

Mwisho, tutambue kuwa kinachoweza kufanyika ndani ya saa moja ya siasa ni sawa na kinachoweza kufanyika ndani ya miaka 10 ya maisha ya kawaida. Yaani, inawezekana kabisa mwaka 2020 upepo huu ukabadilika na majina haya yote yakapotea.

Jiulize hadi Juni 2015, nani alikuwa anahisi kuwa Lowassa aliyekuwa anatajwa na Chadema kuwa ni fisadi, angepewa nafasi ya kugombea urais kupitia chama hichohicho mwezi unaofuata? Lakini Julai mwaka huo, Lowassa alihamia Chadema na kilichotokea ni historia.

Majina yaliyokuwa yanatajwa awali kwenye muungano wa vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa ni Dkt. Wilbroad Slaa (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (Chama Cha Wananchi CUF) ambao wote walitawanyika na kuwa maadui wa Ukawa.

Viongozi wa Ukawa walipokutana Julai 31, 2014 na kuafikiana kuungana katika uchaguzi wa 2015

Je, ni Lowassa au Lissu 2020, nina uhakika hata wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti kwa sasa hawana majibu ya angalau asilimia 90. Na huenda wakajikuta wao pia wanaji-surprise muda ukifika kama ilivyokuwa 2015.

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalando, wiki iliyopita aliishauri Chadema ambacho ni chama chake kuweka mfumo utakaomuwezesha kila mwanachama mwenye sifa na mwenye nia kuwania nafasi ya kugombea, kushiriki kinyang’anyiro cha uteuzi. Huenda hii itaondoa utabiri wa majina kutokana na msimu.

“Chadema wanapaswa kuweka mfumo wenye kuonesha utaratibu mahsusi ambao uko wazi kabisa na wa kidemokrasia. Nashauri hadi mwezi Juni mwaka huu uwe umekamilika kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2020,” Nyalandu anakaririwa.

Tofauti na upande huu wa upinzani, CCM wao ni rahisi kutabiri leo na utabiri wako wa nani atakuwa mgombea urais 2020 ukatimia kwa asilimia 99.9. Nadhani jina unalotaja ndilo nililotaka kutaja pia.

Nilirudishe swali kwako.

Je, kama uchaguzi ungefanyika mwaka huu, kwa kuzingatia hali ya kisiasa ilivyo hivi sasa, nani angepewa nafasi ya kugombea urais kupitia Chadema?

 

Mahakama yahalalisha matokeo ya DRC, mpinzani ang’aka
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 20, 2019

Comments

comments