Na Ghati:

Jana, asilimia 75 ya shughuli zote kwenye mtandao wa Instagram Tanzania zilisimama kwa muda, na kilichokuwa kinaendelea ni mjadala wa nyota ya ‘Pierre Liquid’, aliyejipatia umaarufu kwa kuonesha hisia zake baada ya kunywa bia. Hivyo tu!

Kweli usiache kuonesha hisia zako kwenye kitu ukipendacho, inaweza kuwa ndio tundu lako la kutokea, Pierre alifanikiwa kihivyo tu, kuonesha hisia zake kwenye kile ambacho wengi hukipenda pia, bia aka monde au vitu. Ila akaweka ubunifu ndani yake na kuutumia kuunga mkono kwa nguvu zote ‘vitu vya maana’.

Hakuwahi kufikiria leo angetajwa kwenye hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mama Samia Suluhu Hassan akipewa shukurani, au hata kutajwa kwenye hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika hali ambayo ilimuumiza kwa muda lakini ikampigisha hatua 1000 zaidi. Hii ndio sababu alimuandikia ujumbe wa kumshukuru na kumuombea Mungu ampe kila hitaji la moyo wake, ujumbe ambao hata hivyo aliufuta baadaye, huenda kutokana na ‘comments’ zilizokuwa na njia tofauti na aliyokuwa anamaanisha.

 

View this post on Instagram

 

TANZANIA OYEEEEEEE……. ? CHIIIIIII TANZANIA ITABAKI KILELENI CHIII IMEPAAA HIYOOOOOOOO

A post shared by pierre gumbo (@officialpierre_liquid) on

Tunafahamu kuwa Pierre Liquid alikuwa anapendwa, lakini mimi, naamini hata wewe pia, hukuwahi kujua kama anapendwa kwa kiasi gani na baadhi ya Watanzania hadi juzi alipotajwa na RC Makonda kuwa kati ya ‘walevi’ wasiofaa kupewa nafasi na vyombo vya habari. Baada ya hapo, asiyemjua alimjua, anayemjua alimjua zaidi.

Naomba nisirudie hii stori ya jinsi alivyokula mashavu hadi ughaibuni. Kama anavyopenda kusema Edward Lowassa, “wewe na mimi tunajua, na dunia inajua.” Hata Victor Wanyama, Mkenya anaichezea Tottenham Hotspur ya Uingereza na Ommy Dimpoz wanajua.

 

View this post on Instagram

 

CHIIIIII ETI NINI LAMBA LOLOOO @victorwanyama @ommydimpoz

A post shared by pierre gumbo (@officialpierre_liquid) on


Pierre amekuwa mtu wa kwanza wa kawaida mwaka huu kupata utetezi wa hali ya juu dhidi ya kiongozi mkubwa, akitetewa na viongozi wakubwa, wadogo na watu wa kawaida ambao kwa ujumla wao walionesha kutokubaliana na kauli ya RC Makonda aliyoitoa kwenye tukio la kampeni ya ‘Tokomeza Zero’ iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.

Badala ya kuwa siku ya anguko lake, Pierre Liquid ilikuwa siku ya kupaa kwake kwenda juu zaidi na kubaki kileleni! Aliongoza picha yake kutrend, mashavu yaliongezeka, kila aliyemkosoa ‘aliipatapata’. Unaambiwa mambo ya binadamu [kwa sauti ya Soudy Brown], jamaa alipata mashavu lukuki juzi na jana. Alipewa matangazo zaidi, vyombo vya habari mtandaoni karibu kila kimoja kilipita na pembe (angle) yake ili mradi kisipitwe na trend.

kwani huyu ‘mnywaji’ kawapa nini Watanzania? Majibu ni rahisi…

Mwandishi maarufu wa vitabu kuhusu maisha, Dkt. Elia Gourgourish, katika kitabu chake cha ‘7 Paths to Lasting Happiness’, anasema ‘mafanikio ya juu zaidi katika maisha ya binadamu ni kufurahi’.

Hakuna kitu cha maana zaidi kwa binadamu aliye hai kama ‘kufurahi’. Na hii ndio sababu watu wengi hutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuitafuta furaha tu, kwa sababu ndio mafanikio ya juu zaidi. Hata kama unafanya maajabu na kuijenga dunia kuwa kama mbingu, kama mwisho wake haitaleta furaha basi halina maana. Na kama una pesa nyingi lakini hauna furaha, bado utateseka sana zaidi ya kapuku.

Ndio maana soko la komedi ni soko la mabilioni ya fedha, na watu wanaowachekesha watu ni matajiri wakubwa duniani. Wanafanya vitu vinavyoonekana vya ‘ajabu-ajabu’ lakini kama vinawachekesha watu bila kuvunja sheria na maadili, hiyo ni biashara kama kiwanda. Pierre Liquid, amefanikiwa kwenye hili baada ya kula vitu vyake, anawakusanya watu anawafurahisha kwa vimisemo vya kawaida vinavyochekesha kutoka kwa mnywaji.

“Mimi napenda watu wafurahi, nikishakunywa vitu vyangu huwa nataka kuwafurahisha watu tu, tunywe tufurahi, sipendi kabisa kumuudi mtu,” Pierre alifunguka akiwa Kenya.

Pili, ametumia umaarufu wake kwenye baadhi ya masuala ya msingi. Umaarufu wake umekuwa mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, lakini amefanikiwa kuutumia kuongeza thamani kwenye kampeni kubwa za maana. Mfano, amefanikiwa kuhamasisha watanzania kuiunga mkono Taifa Stars, amefanikiwa kutoa mchango wake kwenye kampeni muhimu kama ‘Tokomeza Zero’.

“Kipekee kabisa nimshukuru @officialpierre_liquid wako watu maarufu wengi mno tuliowaalika lakini hawakufika. Ila wewe ulichukua muda wako kuhamasisha na kufika na zaidi ya hapo ukatoa mchango wa Tsh. Lakini Moja! Haukuja kuuza sura tu, nasema ASANTE SANA,” Mkuu wa Wilaya, Jokate alimuandikia.

Hali hiyo ndiyo iliyomfanya kupata Baraka za shukurani kutoka kwa Makamu wa Rais, Mama Suluhu Hassan kwa jinsi alivyochangia kuhamasisha ushindi wa Stars.

Tatu, amegusa wengi wanapopajua. Sio suala geni kupata mchekeshaji ‘mlevi’, mtakumbuka kuna wengi sana hutumia ulevi kuwachekesha watu, lakini wao huwa hawanywi, wanaigiza tu. Pierre yeye ametumia uhalisia, anakunywa kweli na anachekesha kwa namna yake. Matokeo ya kunywa kwake hayakeri waliomzunguka wakati huo.

Nne, amefanikiwa kupata ‘huruma ya Watanzania’. Ndivyo wengi wanavyoweza kusema, hatuoni moja kwa moja kikubwa kinachompa mashavu Pierre. Lakini wengi wanamini pia kuwa alikosewa, aliumizwa hadharani. Hivyo, huruma yao imekuwa chombo cha kumpeperusha zaidi. Sasa anatetewa na wengi, tena amepata utetezi kutoka kwa watu wenye ushawishi mkubwa Serikalini ikiwa ni pamoja na Mawaziri, wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii na watu wa kawaida.

Kwa mantiki hii, atabaki kuwa juu, ubalozi wa bidhaa mbalimbali utaendelea kumiminika hadi pale ubunifu wake utakapofikia kikomo na watu kumuona wa kawaida tu. Siku watu watakavyomuona kama ‘mlevi tu’, ndipo mwisho wake utakapoishia. Lakini naamini hajapata umaarufu kwakuwa ni mlevi tu. Ni walevi wangapi tunawaona na tunaishi nao hawajawa maarufu? Tena walevi konki! Lakini John Walker alikuwa muimbaji muigizaji tu wa ulevi lakini akawa maarufu kwa alichokuwa anakisema, na hiyo ikawa ajira yake!

Klint Da Drunk, mchekeshaji maarufu wa Nigeria, hatumii pombe yoyote anapopanda jukwaani, lakini anazungumza kama mlevi tu na anachozungumza kinawafurahisha watu na kumpa mamilioni ya fedha. Hivyo, ulevi sio issue kwenye hili. Ubunifu ndio issue, japo unawakwaza wengi.

Inaweza kukuumiza kuona umeandika kitabu kwa miaka mitano, umezunguka nchi nzima unafanya research na kugundua madini ya Tanzanite lakini unazidiwa umaarufu na Pierre! Ni kawaida, wewe unaweza usiwe maarufu lakini una fungu lako pia, kubwa na mchango wako mkubwa katika kutafuta mafanikio ya juu zaidi ambayo ni ‘furaha’.

Dunia inazunguka kwa sababu nyingi. Tusiunge mkono ulevi wa aina yoyote kwani hata vitabu vitakatifu vinakataza. Lakini ukweli ni kwamba Watu wengi sana wapenda pombe. Sijui kwanini!? Mimi bahati nzuri/mbaya umri bado haujaruhusu kunywa vilevi. Lol!

Lakini niligundua hilo siku ile RC Makonda alipotangaza kuwa Taifa Stars ikishinda bia zitauzwa nusu bei jijini Dar es Salaam… wacha, nasikia eti kuna walio safiri kutoka mikoani ili kuwa sehemu ya ofa hiyo. Bia ina nini hii jamani! Ningekuwa mkubwa ningejaribu kizibo kimoja… naamini haitakuwa ile ya ‘ukionja asali….’

Nguvu ya mitandao ya kijamii nayo imefanikiwa kuwabeba wengi, na wakati mwingine ni kama hivi ambavyo kwa kawaida, baada ya kauli ya RC Makonda, Pierre alipaswa kuanguka lakini tunaona amepaa zaidi. Kilichombeba na kumpaisha ni hayo niliyoeleza juu lakini yasingewezekana bila nguvu ya mitandao ya kijamii. Mitandao hii inaweza kulichukua dogo likawa kubwa, kubwa likawa dogo. Usiichukulie poa!

Cha msingi wote tuombe wote tubaki kuwa juu, tubaki kuwa kileleni kwenye furaha…chiiiii (kwa sauti ya Pierre).

Video: Inasikitisha, azaliwa na matundu usoni, familia yamtenga, mama afunguka
Video: NEC yapuliza kipenga uchaguzi wa Arumeru, Makonda achafua hewa