Serikali imewataka Watanzania kutokuwa na wasiwasi kwani mwenendo wa uchumi ni wa kuridhisha na unaendelea kuimarika. Aidha, tathmini iliyofanyika kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya fedha, inaonesha kuwa Mabenki yetu bado yapo salama.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Septemba 16, 2016 wakati akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge Jijini Dodoma.

Kufuatia hali ya wasiwasi kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi, hususan mtiririko wa fedha kwenye uchumi wa Taifa Waziri Mkuu amesema tathmini iliyofanyika kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya fedha, inaonesha kuwa Mabenki yetu bado yapo salama, na yana mitaji ya kutosha na mwenendo wa sekta ya fedha ni wa kuridhisha. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ya Taifa ya Takwimu zinafuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi Nchini.

Majaliwa amesema hali ya uchumi wetu ni shwari kabisa na si mbaya kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu, ambapo tarehe 14 Septemba, 2016 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini na kulihakikishia Taifa na Jumuiya ya Kimataifa.

Majaliwa ameeleza kuwa katika taarifa hiyo ya Benki Kuu pamoja na mambo mengine, imebainishwa kwamba katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa wa kuridhisha. Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka 2015.

Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za mawasiliano, utangazaji na huduma ya intaneti; kuongezeka kwa uchimbaji na madini. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu katika kipindi hicho ni sekta ya fedha kwa asilimia 13.5, mawasiliano asilimia 13.4 na utawala wa umma asilimia 10.2.

Majaliwa amesema kufuatia mwenendo huo mzuri wa viashiria vya shughuli za uchumi, ni dhahiri kwamba mwelekeo wa uchumi katika kipindi kijacho unatoa matumaini ya uchumi kuendelea kuimarika kama ilivyokadiriwa hapo awali na kufikiwa kwa lengo la ukuaji wa pato la Taifa la asilimia 7.2 kwa mwaka 2016.

Kutokana na matumaini ya uchumi kuimarika, Majaliwa amesema ni ukweli kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri katika kuimarisha uchumi endelevu, usimamizi thabiti wa rasilimali za umma, na ujenzi wa miundombinu bora yenye kuimarisha lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Waziri Mkuu apokea sh. mil. 121.679 kusaidia waathirika tetemeko la ardhi Kagera
Vyanzo vitano vya bahati mbaya.

Comments

comments