Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Mkuu wa wilaya ya Biharamulo, Sada Malunde na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Wende Ng’ahara wamalize tofauti zao na wasipojirekebisha atamshauri Rais Dkt. John Magufuli kufanya maamuzi mengine.

Amesema kuwa kitendo cha viongozi hao kutoelewana kinaonyesha mfano mbaya kwa watumishi walio chini yao, hivyo amewataka wajirekebishe mara moja kwani wameaminiwa na Serikali kuliongoza eneo hilo na si kuwachanganya wananchi.

Ametoa agizo hilo wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyakanazi, Biharamulo mkoani Kagera, ambapo amesema kuwa kutoelewana kwa viongozi hao ambao wakati mwingine wanatuhumiana kufanyiana vitendo vya kishirikina kumesababisha kuzorota kwa shughuli za maendeleo katika wilaya hiyo.

“Mliletwa hapa kuiwakilisha Serikali na kusimamia maendeleo ya wananchi nyie mnagombana. nawataka sasa mmalize tofauti zenu ili muweze kufanyakazi za maendeleo, kama hamtafanya hivyo nitamshauri Rais Dkt. Magufuli,”amesema Majaliwa

Aidha, akiwa njiani kuelekea mkoani Kagera alitembelea kambi ya Nyanza Roads inayojenga barabara ya Nyakanazi-Kabingo, inayounganisha mikoa ya Kigoma na Kagera na kusema kuwa hajaridhishwa na kasi ya mkandarasi huyo.

“Sijaridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hii, mkandarasi na mhandisi mshauri wote wanaonekana hawapo makini katika kufanya kazi hii. Hii ni aibu kwa wakandarasi wa ndani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia kutokupewa kazi kumbe hawako makini.”amesema Majaliwa

Hata hivyo, Barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami ina urefu wa kilomita 50 na ilianza kujengwa 2014 ilitarajiwa kukamilika 2016, ambapo kwa sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 60.

 

Video: Rais Trump adata na danadana za mwanamke Mtanzania, afunguka
Uchafuzi wa Fukwe Manispaa ya Lindi kutafutiwa ufumbuzi