Waziri Mkuu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa vituo vya kulea watoto wasiofuata taratibu za usajili, wanaowatumia watoto kama mitaji au kwa maslahi binafsi na wanaoendesha shughuli hiyo kwa minajili ya kidini na kikabila.

Amewataka pia wamiliki hao waache mara moja kuwalea watoto katika maadili yasiyofaa na yasiyo ya Kitanzania na kwamba maofisa ustawi wa jamii wahusike moja kwa moja katika usajili wa mtoto ili kuhakikisha wanakuwa na watoto wanaostahili tu kuwekwa kwenye makao ndiyo wanaosajiliwa.

“Nitoe rai kwa mtu mmoja mmoja, taasisi na makao wazingatie baadhi ya taratibu za msingi za uendeshaji wa makao kama vile mtoto kukuzwa katika mazingira ya familia, kuzingatia misingi ya kitaifa badala ya misingi ya tamaduni za kigeni,”amesema Majaliwa

Amesema kuwa mtoto hukuzwa kwa kuzingatia maslahi bora ya mtoto, kuzingatia umuhimu wa kuwa na mwendelezo katika dini ya mtoto na utamaduni wake, kutotenganisha watoto na ndugu na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma stahiki, kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji pamoja na kutunzwa na  kuendelezwa hadi kufikia kimo cha utimilifu wao.

Aidha, Majaliwa amewataka wamiliki wa taasisi na makao, kuwaruhusu maafisa ustawi wa jamii na maafisa wengine wa Serikali wafanye ukaguzi kwa mujibu wa sheria na waweke utaratibu wa kuandaa taarifa za kila mwezi za watoto na taarifa ya mwaka wa fedha.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameongeza kuwa taasisi na makao zihakikishe kuwa kila mtoto anawekewa mpango maalumu wa kuondoka kwenye makao na namna ya kumuunganisha mtoto huyo na familia yake.

 

Marufuku ya mifuko ya plastiki kuibua fursa ya kiuchumi
Ruhusa ya Utoaji Mimba Greenland yageuka Mwiba