Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa maamuzi ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kuwa Jiji ni sahihi na ameyafanya kwa wakati muafaka na hakuna sheria iliyokiukwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 3, 2018) Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 21 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu, Felista Bura ambapo alitaka kupata kauli ya Serikali juu ya baadhi ya watu wanaobeza maamuzi ya Rais Dkt. Magufuli ya kuupandisha hadhi mji wa Dodoma.

“Rais Dkt. Magufuli hakukiuka sheria kwa sababu ana mamlaka kwa mujibu wa katiba ibara 2 na sheria ya Mamlaka ya serikali za Mitaa sura ya 288 kupandisha hadhi mji au eneo lolote kadiri ya mahitaji yatakavyohitajika. hata kitendo cha Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali pamoja na upatikanaji wa miundombinu muhimu kama ya afya, maji, umeme, barabara na kuendelea kukua kwa ukusanyaji mapato ni vigezo tosha vya kuufanya mji wa Dodoma kuwa Jiji,”amesema Majaliwa

Hata hivyo, Aprili 26, 2018 Rais Dkt. Magufuli aliupandisha hadhi mji wa Dodoma kutoka Halmashauri ya Manispaa na kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na kumteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

 

Romelu Lukaku atibiwa Ubelgiji, kukosa mchezo wa kesho
Bruno Martins Indi kuwasubiri Swansea City