Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Thomas Chogolo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za ubadhilifu wa makusanyo ya mapato ya halmashauri hiyo.

Pia, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa halmashauri hiyo kumaliza haraka migogoro yao ya kiutendaji kabla ya Serikali haijawachukulia hatua kwani wanachokifanya ni kinyume na maelekezo yake.

Amechukua hatua hiyo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma.

”Katika Serikali hii suala la ukusanyaji wa mapato ni jambo nyeti na limepewa kipaumbele, hivyo ni lazima fedha inayokusanywa itumike kama ilivyokusudiwa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.”amesema Majaliwa

Aidha, amesema kuwa wananchi wa halmashauri hiyo wanalipa kodi kupitia kwa watendaji wa kata katika maeneo yao lakini Mweka Hazina haingizi kwenye mfumo wa Serikali.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameongeza kuwa uaminifu na uadilifu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na watumishi wa umma, hivyo amewataka watumishi hao wasijiingize kwenye mambo ambayo hayana tija katika utumishi wao.

Kangi Lugola amng'oa mkuu wa kituo cha Polisi Mang'ola
Zamaradi aguswa gharama matibabu ya Ruge, ahamasisha michango