Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa kuibuka kwa sekta za mafuta na gesi hapa nchini kumeleta haja ya kuwa na wabobezi wa masuala hayo katika taaluma ya sheria.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wageni mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

Amesema uzinduzi wa ofisi hizo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhamishia makao makuu ya nchi jijini Dodoma.

“Taaluma ya sheria kwa sasa inahitaji kuwepo kwa ubobezi. Imekuwa si rahisi tena kwa mwanasheria kuwa na utaalamu wa kutosha katika maeneo yote ya sheria. Hii inatokana na ukweli kuwa taaluma ya sheria imepanuka na masuala mapya kama vile mafuta, gesi, haki bunifu na makosa ya kimtandao yamekuwa yakijitokeza kila kukicha,” amesema Majaliwa.

Hata hivyo, Majaliwa ameongeza kuwa Ofisi hizo ni matokeo ya juhudi za makusudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anazochukua katika kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini na kuimarisha ulinzi wa maliasili na utajiri wa Taifa kwa kuunda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

 

Chile, Peru wenyeji wa fainali za klabu Amerika kusini 2019
Luciano Spalletti atamani kufanya kazi na Modric