Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini katika kutimiza azma yake ya kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.

Amesema kuwa Tanzania inahitaji uungwaji mkono na Serikali ya Afrika Kusini hususani katika kipindi hiki ambacho imedhamiria kuimarisha shughuli za uzalishaji kupitia viwanda kwa lengo la kufikia uchumi wa kati..

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Agosti 16, 2019) wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus ya Morogoro.

Amesema kuwa kwa kuwa changamoto zinazoikabili Tanzania katika nyanja mbalimbali zinafanana na zile za Afrika Kusini kwani historia za nchi hiyo na Jiografia vinafanana na Serikali ya Tanzania.

Akizungumzia kuhusu eneo la Mazimbu, Majaliwa amesema kuwa lina uhusiano mkubwa na historia ya nchi hizo mbili kwa sababu huwezi kuulezea vizuri uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini pasi na kulitaja eneo hilo.

Waziri Mkuu amesema eneo la Mazimbu limebeba historia muhimu ya kumbukumbu ya vuguvugu la ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

“Mheshimiwa Rais, Tanzania ikishirikiana na nchi tano zilizokuwa katika kundi la mstari wa mbele (Angola, Tanzania, Zambia, Botswana na Msumbiji) ilijishughulisha sana katika ukombozi kusini mwa Afrika na katika kukomesha sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini,”amesema Majaliwa

Kwa upande wake, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa mchango mkubwa ilioutoa kwa nchi ya Afrika Kusini wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo, hivyo wataendelea kuimarisha ushirikiano.

Rais huyo wa Afrika Kusini amesema kuwa Serikali yake ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali na kukuza teknolojia.

Rais Ramaphosa aliwasili katika uwanja wa ndege wa Morogoro saa 4.21 asubuhi na kupokelewa na Waziri Mkuu. Kisha alitembelea Campus ya Solomon Mahlangu na kujionea maeneo ambayo wapigania uhuru wa Afrika Kusini walikuwa wakikutana na kupanga mipango mbalimbali.

Pia kiongozi huyo ambaye kwa mara ya kwanza amefika mkoani Morogoro leo alitembelea campus ya Mazimbu na kujionea sehemu ambazo waliishi wapigania uhuru wa nchi yake na kisha aliweka shada la maua kwenye makaburi ya wapigania uhuru.

Airport Terminal 3 yawapagawisha mabalozi, watoa ahadi lukuki
Marekani yaweka vikwazo dhidi ya mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Sudan