Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, dkt. John Pombe Magufuli amewashukuru viongozi wa dini na watanzania wote kwa kuitikia wito wa kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Magufuli ametoa shukrani hizo leo tarehe 07 Juni, alipokaribishwa kuwasalimu Waumini wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Chamwino mkoani Dodoma baada ya kuhudhuria Misa Takatifu ya Sikukuu ya Utatu Mtakatifu iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padre Paulo Mapalala.

Amesema Mwenyezi Mungu amejibu maombi ya watanzania ambao wamesali, wamefanya toba na kufunga, na matokeo yake ni kuwa maambukizi ya virusi vya Corona yamepungua, na wananchi wanaendelea na maisha yao huku wakichapa kazi za uzalishaji mali, tofauti na ilivyodhaniwa kuwa ugonjwa huo ungesababisha madhara makubwa.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuwa makini dhidi ya mbinu zozote zinazoweza kufanywa kuwaambukiza ugonjwa huo ama magonjwa mengine, huku wakimshukuru na kumtumaini Mwenyezi Mungu aliye muweza wa yote.

Aidha akiwa Kanisani hapo Mhe. Rais Magufuli ameendesha harambee ya kuchangia upanuzi wa Kanisa hilo na kufanikiwa kuchangisha shilingi Milioni 17,229,000/- (ikiwemo shilingi Milioni 10 aliyochangia yeye mwenyewe) na mifuko 76 ya saruji, na ametaka upanuzi wa Kanisa hilo uanze kesho.

Wami: Ajali mbili za lori zatokea kwa mpigo na kusababisha vifo
Mtandao kusaidia maonesho ya sabasaba 2020