Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli ameendelea kupokelewa kwa mikono miwili na kukubalika kwa wananchi wa mikoa ya kusini alikopita kuomba kuomba kura.

Magufuli ambaye amevuta umati mkubwa wa watu katika mikoa hiyo huku akipewa heshima ya kipekee kwa kutandikiwa vitenge na akina mama ili apite, ameahidi kufanya mabadiliko makubwa na kushughulikia kikamilifu ufisadi.

Akiongea katika mikutano yake, Magufuli ambaye kutokana na utendaji wake hivi sasa anaitwa ‘tingatinga’ amesema kuwa anashangazwa kuona wanafunzi wanakaa chini darasani wakati  taifa limejaliwa kuwa na misitu mikubwa.

Kutokana na hali hiyo aliahidi kuwa atahakikisha hakuna mwanafunzi nchini anayekosa dawati huku akisisitiza ahadi yake ya elimu bure hadi kidato cha nne.

“Najua watu watasema nitatoa wapi hela, nchi yetu ina mapato mengi sana ila kuna wajanja kule juu serikalini wanafanya tofauti, sasa nataka nikapambane nao hukohuko,” alisema Magufuli.

Katika hatua nyingine, Magufuli amewahidi watanzania kuwa serikali yake itahakikisha inajali makundi maalum wakiwemo kuboresha maisha ya wazee hususani penseni za uzeeni.

Aliwaahidi wakazi wa mikoa hiyo ya kusini kuwa atahakikisha anatatua tatizo la maji na kufuta tamasha la wiki ya maji ambalo anaona halina tija kwa kuwa hutumia fedha nyingi zinazozidi hata mahitaji ya fedha za miradi ya maji.

“Waziri wa maji nitakayemteua atakuwa na kazi ya kuleta maji sio kila siku tuko kwenye mchakato. Akiwa na lugha hii itabidi akae pembeni ili akajichakatue mwenyewe, hili sikubali hata kidogo,” alisisitiza.

Mgombea huyo hakuisahau ahadi ya kuwaboreshea wakulima mazingira mazuri ya kuuza mazao yao kwa serikali na kwamba itakuwa mwiko kwa serikali yake kuwakopa wakulima.

Ameendelea kusisitiza kuwa atakapoingia madarakani ataunda baraza dogo la mawaziri wachapakazi usiku na mchana na kwamba kwake itakua ‘kazi tu’.

 

Makundi Ya Ligi Ya Mabingwa Wa Ulaya Yaanikwa
Lowassa, Magufuli Uso Kwa Uso Kwenye Mdahalo