Muungano wa Taasisi zinazopambana dhidi ya unyanyasaji/ukatili wa kijinsia (MKUKI), umesema kuwa unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana umeongezeka duniani kote, wakati huu wa mapambano dhidi ya virusi vipya vya corona (covid-19).

Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF), Anna Kulaya amesema wakati akisoma tamko la pamoja na MKUKI kuwa uamuzi wa kuwafungia ndani watu (lockdown) au hata kuweka sheria kali za kubaki majumbani katika baadhi ya nchi, kulisababisha mrundikano wa watu majumbani.

Alisema kuwa hatua hiyo imechochea ongezeko la unyanyasaji wa kijinsia na ukatili ulioripotiwa duniani kote.

“Kwa mfano, Ufaransa imeripoti ongezeko la asilimia 30 la unyanyasi wa kijinsia katika kipindi cha ‘lockdown’ hadi Machi, 2020. Hali inafanana hivyo katika nchi za Singapore (33%), Cyprus (30%) na Argentina (25%),” alisema Kulaya.

Ameongeza kuwa kutokana na hali ilivyo sasa, Tanzania pia haikusalimika katika ongezeko hilo, na kwamba kuna ulazima wa kuchukua hatua kupambana na tatizo hilo sasa.

Kabla ya mlipuko wa corona, Umoja wa Mataifa walisema mmoja kati ya wanawake watatu atakumbwa na unyanyasaji majumbani; na sasa wanawake hao wamewekwa nyumbani wakati wote na ‘watesi’ wao, hali inayoongeza uwezekano wa kunyanyaswa zaidi.

Mkurugenzi huyo wa WiLDAF ameeleza kuwa wanawake hao wengi wamejikuta hawana msaada kwakuwa wako majumbani muda wote, na huko nje wanaona hakuna namna ya kupata msaada wa haraka kwani mashirika mengi yamefungwa au yameelemewa na kesi mpya za unyanyasaji majumbani.

Waziri Mkuu ataja idadi mpya ya wagonjwa wa corona

Katavi: Mtuhumiwa ubakaji auawa kwa fimbo

Corona ilivyopelekea kukamatwa mtuhumiwa mauaji ya kimbari Rwanda, kesi kusikilizwa Tanzania
Burundi: Matokeo ya awali ya uchaguzi kutangazwa leo